Zanzibar yapata medali mbili za Dhahabu Umisseta

WACHEZAJI wa mpira wa Wavu mashindano ya Umisseta kanda ya Unguja wakijaribu kuzuwia mashambulizi wakati wa mchezo wao dhidi ya Mbeya ambapo, Unguja ilifungwa seti 3-1.

TIMU za Zanzibar zinazoshiriki mashindano ya umoja wa michezo kwa skuli za sekondari Tanzania (Umisseta),zinaendelea kufanya vyema baada jana kushinda kwenye michezo tofauti ikiwemo riadha.

Mchezo wa mpira wa mikono wanaume wameshinda mabao 35-14 dhidi ya Lindi mchezo mabao ulikuwa mzuri na Unguja kutawala kwa muda mrefu mchezo huo, ambapo hadi mapumziko ilikuwa ikiongoza kwa mabao 20-6.

Kwa upande wanawake Unguja imekubali kichapo cha mabao 22-10 dhidi ya Morogoro, mchezo ambao Unguja italazimika kujilaumu yenyewe kwa kushindwa kutumia nafasi nyingi za kufunga walizozipata.

Mchezo wa Wavu kanda ya Pemba imetoka na ushindi wa seti 3-1  dhidi ya Katavi, ambapo katika mchezo huo Pemba ilicheza vyema kulinganisha na mchezo wa awali baada kurekebisha makosa kadhaa yaliyojitokeza mchezo wa kwanza ambao ilipoteza, wakati Unguja wao walishinda kwa seti 3-0 dhidi ya Rukwa.

Kwa upande wa mpira wa miguu matokeo hayakuwa mazuri kwa michezo ya awali ambapo Unguja ilivutwa shati na Dodoma baada ya kutoka sare ya bila ya kufungana, huku Pemba ikakubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Katavi,mchezo ambao Pemba watajilaumu wenyewe kwa kushindwa kutoka na ushindi baada ya kutawala muda mrefu, lakini walishindwa kutumia nafasi walizopata.

Kwa mchezo wa netiboli Unguja imekubali kichapo cha mabao 21-12 dhidi ya Mkoa wa Dodoma ,mchezo ambao Unguja ilionyesha upinzani kiasi lakini walishindwa kutumia nafasi walizozipata.

Mchezo wa Wavu baada ya jana Pemba wanawake kutoka na ushindi wa seti 3-1 dhidi ya Mara, jana walikubali kichapo cha seti 3-2 dhidi ya Pwani, mchezo ambao ulikwa wa vute nikuvute kwa muda wote.

Nayo timu ya mpira wa Kikapu ya Unguja imeendeleza wimbi la ushindi baada ya kuilaza bila ya huruma timu ya Mkoa wa Mara kwa vikapu 48-10, leo Unguja itacheza mchezo wa tatu dhidi ya Morogoro ambapo kama itashinda itaanza kunusa kuingia hatua ya robo fainali.

Kwa upande wa mchezo wa kurusha tufe Unguja ikafanikiwa kupata medali ya dhahabu baada ya mchezaji Samir Mbaraka Sururu kurusha umbali  wa mita 12.Sentimita 84, mchezo wa kuruka juu Dioniez Nyamsha Mneno amepata medali ya dhahabu. Michezo ya riadha mita 200 wanaume na wanawake wameingia hatua ya pili, na wanaume mita 400.

error: Content is protected !!