Zaidi ya Wapalestina milioni moja Ghaza kukosa chakula ifikapo Juni

Zaidi ya Wapalestina milioni moja katika Ukanda wa Ghaza, yaani takribani nusu milioni ya wakazi wa eneo hilo, huenda wasiwe na chakula ifikapo mwezi Juni mwaka huu.

Tahadhari hiyo imetolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA.

Kwa mujibu wa taarifa ya UNRWA iliyotolewa wakati huu ambao Waislamu wote kote duniani wako katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, aghalabu ya wakaazi wa Ukanda wa Ghaza wanategemea msaada wa chakula kutoka kwa jamii ya kimataifa, na endapo UNRWA haitopata fedha za ziada takriban dola milioni 60 ifikapo Juni, basi uwezo wa shirika hilo kuendelea kutoa misaada kwa wakimbizi zaidi ya milioni moja wa Kipelestina Gaza, wakiwemo 620,000 wanaohesabika kuwa ni hohehahe wasiojiweza hata kumudu mahitaji ya msingi ya chakula na kulazimika kuishi kwa chini ya dola 1.6 kwa siku na pia watu wengine 390,000 masikini, watakabiliwa na hatari kubwa. Akisisitiza kuhusu hali hiyo, Maththias Schmale, mkurugenzi wa operesheni wa UNRWA amesema “Watu hawana muelekeo, asilimia 53 ya watu wanaopaswa kuajiriwa hawana ajira na matumaini ni madogo sana ya kupata ajira, na Gaza ni zaidi ya asilimia 50. Asilimia 80 ya wakimbizi ambao wameorodheshwa kwetu wanaishi chini ya kiwango cha umasikini na wanatutegemea kwa msaada wa chakula.”

Tokea mwaka 2007, utawala haramu wa Israel umeweka mzingiro wa anga, nchi kavu na baharini dhidi ya Ukanda wa Ghaza baada ya Wapalestina katika eneo hilo kuichagua kidemokrasia harakati ya Hamas kuongeza eneo hilo. Mzingiro huo umelifanya eneo hilo lenye watu karibu milioni moja na nusu kutajwa kuwa gereza kubwa zaidi la wazi duniani. Misri inashirikiana na Israel katika kuwawekea Wapalestina mzingiro kwani njia ya nchi kavu inayounganihsa Ghaza na nchi zingine duniani ni kupitia mipaka ya Misri.

Mbali na mzingiro huo, utawala haramu wa Israel pia umeanzisha vita mara tatu dhidi ya Ghaza tokea mwaka 2008 ambapo maelfu ya Wapalestina wakiwemo wanawake na watoto wameuawa mbali na miundo mbinu ya eneo hilo kama vile mahospitali, shule na nyuma za makazi kuharibiwa.

error: Content is protected !!