Wavuvi 103 waliopotea Kenya wapatikana wakiwa salama baada ya wengine 32 kuwasili kisiwani Pemba kwa kutumia meli ya Sea Star I wakitokea Tanga

WAVUVI 79 kati ya 103 waliopotea katika bahari ya Mombasa Kenya, wamepatikana wakiwa salama baada ya wengine 32 kuwasili jana kisiwani Pemba kwa kutumia meli ya Sea Star I wakitokea Tanga.

Wavuvi hao ambao wengi wao wanatoka katika wilaya ya Wete, waliwasili katika bandari ya Wete jana huku wengine 24 waliosalia tayari wamepatikana na wanatarajiwa kurudi nyumbani muda wowote kuanzia sasa.

Akizungumza na wavuvi hao pamoja na jamaa zao waliofika bandarini hapo kwa ajili ya kuwapokea, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Mohammed Ahmada Salum, aliishukuru serikali ya Kenya pamoja na ubalozi wa Tanzania nchini humo kwa uungwana waliouonyesha katika kuokoa maisha ya wananchi hao.

Alisema kitendo walichokionyesha ndugu zao hao wa Kenya ni cha kuigwa, hivyo aliiomba serikali ya nchi hiyo kuendelea kushirikiana katika mambo mbali mbali, yakiwemo ya maendeleo.

Aliwaomba wananchi wote wanaotumia au kumiliki vyombo vya baharini kuweka vyombo vya kujiokoa wakati wanapopata matatizo pamoja na mawasiliano.

“Leo hii hapa tungekuwa tunazungumza vyengine watu wote hawa wangepoteza maisha ingelikuwa msiba mkubwa kwetu,” alisema.

Aliwaomba wenye vyombo vya baharini kuwa na utamaduni wa kusajili vyombo vyao katika mamlaka husika ili kuepusha matatizo yanayoweza kutokea.

“Niwaombe wananchi wote ambao wanamiliki vyombo vya baharini kuvifanyia usajili vyombo vyao katika mamlaka inayohusika ili vitambuliwe,” alisema.

Mapema Ofisa Mdhamini Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Ali Salim Mata, aliipongeza Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar (ZMA) pamoja na ubalozi wa Tanzania kwa ushirikiano waliotoa kuhakikisha wavuvi hao wanapatikana na wanarejeshwa nyumbani salama.

Aliipongeza kampuni ya Sea Ferries ambayo inamiliki meli ya Sea Star I kwa kukubali kuwasafirisha wananchi hao.

“Nitoe angalizo kwa wananchi wote kuwa ofisi yetu iko mstari wa mbele katika kutoa mafunzo ya uokozi pamoja na kujikinga na maafa, kipindi hiki ni kipindi cha mvua, rai yangu kwa wananchi kuwa na utamaduni wa kusikiliza vyombo vya habari juu ya hali ya hewa,” alisema.

Mapema akitoa taarifa na kuwakabidhi wananchi hao kwa uongozi wa serikali, Ofisa kutoka ZMA, Rashid Haji Ali, alieleza kuwa tukio hilo la kupotea watu hao lilitokea kati ya Mei 22 hadi 24 usiku ambapo wavuvi hao walikuwa baharini kuendelea na shughuli zao za uvuvi.

Alisema baada ya kupata taarifa kutoka Kenya, waliwasiliana na Mohammed Ali ili kujua hali za wananchi hao na hivyo kuelezwa kuwa wote wako salama na idadi yao ni watu 103.

“Lakini baada ya hapo serikali ilitutaka tuhakikishe tunawakabidhi wananchi wake wakiwa wazima”, alisema.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!