Watu kadhaa wahofiwa kuuawa katika mripuko wa bomu Somalia

Watu kadhaa wanahofiwa kuuawa katika mripuko wa bomu lililokuwa limetegwa garini, nje ya jengo la serikali katika eneo lenye shughuli nyingi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Mashuhuda wanasema mripuko huo umetokea leo mwendo wa saa tano asubuhi kwa saa za nchi hiyo karibu na makao makuu ya Wilaya ya Wardhingley, na kwamba watu wengine kadhaa wamejeruhiwa.

Mripuko huo umetokea mita chache kutoka Ikulu ya Rais ya Mogadishu inayofahamika kama “Villa Somalia”.

Shambulio hilo linaonekana kuwa la ulipizaji kisasi, kwa kuwa limejiri siku chache baada ya jeshi la Somalia kuwaua magaidi 18 wa al-Shabaab katika mji wa Jilib uliopo mkoani Juba.

Baada ya kujiri mripuko huo wa leo, wingu jeusi lilitanda angani katika eneo hilo na kufuatiwa na milio ya risasi.

Raia na maafisa usalama wakikimbilia usalama wao baada ya mripuko

Hakuna kundi lililotangaza kuhusika na shambulio hilo kufikia sasa, lakini genge la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limekuwa likitekeleza hujuma za namna hii mara kwa mara hususan katika mji mkuu Mogadishu.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, watu 15 waliuawa katika shambulizi la kigaidi la al-Shabaab katika mji mkuu huo wa Somalia.

Tangu mwaka 2007 kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limekuwa likifanya juhudi zenye lengo la kuipindua serikali kuu ya nchi hiyo ambayo inapata himaya kutoka kwa askari wa Umoja wa Afrika AMISOM.

error: Content is protected !!