Wapinzani waishtaki serikali ya Tanzania katika mahakama ya Afrika Mashariki

Vyama vinne vya upinzani nchini Tanzania vimeishtaki serikali ya Rais John Pombe Magufuli katika mahakama ya Afrika Mashariki kuhusu haki ya EACJ kufuatia mabadiliko ya hivi majuzi ya sheria ya vyama vya siasa.

Sheria hiyo ambayo ilitiwa saini na Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Februari na kuchapishwa katika gazeti la serikali siku 10 baadaye, imezua mjadala mkubwa nchini humo.

Akizungumza jijini Dar es salaam kwa niaba ya vyama vinne vya kisiasa, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe amesema kuwa, malalamishi hayo yamesajiliwa na mahakama ya Afrika Mashariki kuhusu haki ya EACJ.

Hayo yanajiri siku chache tu baada waziri kivuli wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza Liz Mclnnes kuelezea kusikitishwa kwake na kupitishwa kwa sheria ya vyama vya kisiasa nchini Tanzania ambayo anadai inabinya na kukandamiza vyama vya upinzani.

Vyama vya upinzani na asasi za kirai vimekuwa vikilalamikia sheria hiyo vikieleza kwamba, inafanya shughuli za siasa kuwa kosa la jinai. 

Bunge lilipasisha muswada huo mwezi Januari mwaka huu na hatimaye kusainiwa kuwa sheria na Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Licha ya kupongezwa kwa hatua mbalimbali za maendeleo zilizochukuliwa na serikali yake, zikiwemo za kustawisha miundombinu ya kiuchumi na kupambana na ufisadi, Rais wa Tanzania anakosolewa kuwa anaminya demokrasia sambamba na kuendesha kampeni ya kuua vyama vya upinzani nchini humo.

error: Content is protected !!