Wanazuoni 80 wa Kiislamu wa nchi za Magharibi waitaka Saudia isiwanyonge maulama

Wanazuoni 80 wa Kiislamu wanaoishi katika nchi za Magharibi wameuandikia barua utawala wa kifalme wa Saudi Arabia wakiutaka usitekeleze hukumu ya kifo dhidi ya maulama watayu wa nchi hiyo wanaoshikiliwa gerezani.

Jarida la The Economist linalochapishwa nchini Uingereza limeandika kuwa, barua hiyo imeandikwa kwa ubunifu wa msomi wa Kipakistan anayeishi Canada, Faraz Rabbani. 

Wasomi hao wa Kiislamu wameandika barua hiyo baada ya utawala wa Saudi Arabia kuchukua uamuzi wa kuwanyonga maulama watatu wa nchi hiyo ambao ni Sheikh Salman al-Ouda, Sheikh Awad al-Qarni na Ali al-Omari. 

Sheikh Salman al-Ouda alikamatwa na kufungwa jela mwaka 2017 baada ya kuandika ujumbe katika mtandao wa kijamii wa Twitter akisisitiza udharura wa kufanyika suluhu na mapatano baina ya Saudi Arabia na Qatar.

Sheikh Awad al-Qarni ambaye ni mwandishi, mhubiri na mhadhiri wa chuo kikuu na mwenzake Ali al-Omari walitiwa nguvuni Septemba mwaka 2017.

Wapinzani wa utawala wa kifalme wananyongwa Saudia

Tangu Muhammad bin Salman alipoteuliwa kuwa Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia tarehe 21 Juni mwaka 2017 maulama, wasomi na wanaharakati wa masuala ya kijamii wamekuwa wakikabiliwa na mbinyo na ukandamizaji mkubwa nchini humo.

Ripoti zinasema kuwa tangu mwezi Septemba mwaka 2017 hadi Septemba 2018 askari usalama wa Saudia wamewatia nguvuni zaidi ya maimamu na mahatibu mia moja wa misikiti nchini humo.   

error: Content is protected !!