Wanawake wa Israel waandamana kulalamikia ukatili wa kingono

Maelfu ya wanawake wa Israel walifanya maandamano jana Jumanne katika kila kona ya utawala huo haramu, wakilalamikia unyanyasaji wa kingono, mateso dhidi yao na udhalilishaji wa kijinsia.

Maandamano hayo yameambatana na mgomo, ambapo wanawake hao wametangaza kususia kwenda kazini, wakilalamikia ongezeko la visa vya wao kuuliwa, kubakwa, kuteswa na kukandamizwa; wiki mbili baada ya wasichana wawili kuuliwa katika mazingira ya kutatanisha.

Wanawake hao waandamanaji wa Israel walikuwa wamebeba mabango yenye nambari 24, kuashiria idadi ya wanawake waliouawa katika mazingira tatanishi tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, huku wengine wakiwa na mabango yenye ujumbe usemao; “Netanyahu zinduka, damu zetu zina thamani”.

Waandamanaji hao walimwaga rangi nyekundu mabarabarani, kuashiria kushtadi umwagaji damu dhidi ya wanawake wa utawala huo pandikizi.

Dhulma, udhalilishaji wa kingono na mateso dhidi ya wanawake sio mambo mageni kwa Wazayuni ambao kwa miaka mingi sasa wamekuwa na mienendo mibaya kwa wanawake wa Palestina.

Ripoti ya hivi karibuni ya Kamisheni ya Wafungwa wa Kipalestina ilibanisha kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umewatia mbaroni wanawake wasiopungua 15,000 wa Kipalestina tokea mwaka 1967 hadi sasa na unawazuilia katika mazingira ya kutisha, bali hata kuwabaka na kuwapiga.

error: Content is protected !!