Wakusanya takwimu watakiwa kuwa waadilifu

MKUU wa Mkoa wa kusini Pemba Mhe: Hemed Suleiman Abdalla,

UPATIKANAJI wa takwimu na taarifa  sahihi zitakazotumika katika mipango ya maendeleo inayofanywa na serikali, itategemea na wadadisi wenyewe kufanya kazi kwa weledi na kufuata maelekezo waliyopatiwa.

Hayo yalielezwa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Hemed Suleiman Abdalla, katika ukumbi wa baraza la mji wa Chake Chake, wakati akifungua mafunzo ya siku 18 kwa wadadisi wa matumizi ya mapato na matumizi ya kaya kisiwani hapa.

Aliwataka wadadisi hao kuwa makini pale wanapofanya kazi hiyo ili kupata takwimu sahihi ambazo zitaisaidia serikali katika kupanga mipango ya matumizi kwa maslahi ya maendeleo ya taifa.

Alisema serikali inaendelea kufanya jitihada ili kuhakikisha inakuza uchumi na kuondoa

umaskini kwa kupanga mipango itakayotoa takwimu za mambo mbali mbali.

Alieleza mikakati ya kufikia malengo hayo ni pamoja na uandaaji wa dira ya maendeleo ya 2020, ambayo iliandaliwa mwaka 2000 kwa kuweka malengo ya kuondosha umaskini ifikapo mwaka 2020.

Alisema katika kufuatilia na kupima utekelezaji kupitia mpango wa muda mfupi wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Zanzibar (MKUZA) wa mwaka 2005 na baadae MKUZA II mwaka 2010 na hivi sasa  MKUZA III tathmini yake itakwenda

sambamba na dira ya maendeleo ya Zanzibar.

“Nawaomba wadadisi muwe makini pale mnapofanya udadisi katika kutafuta mambo mbali mbali na kujiridhisha kwa vile takwimu mtakazozikusanya ni muhimu kwa maslahi ya taifa katika kufanya mipango ya maendeleo,”alisema.

Alieleza ushahidi wa kitakwimu uliotokana na matokeo ya tafiti za mapato na matumizi ya kaya (HBS) zilizotangulia zinaonyesha Zanzibar imepiga hatua katika jitihada za kuondoa  umaskini.

Alisema utafiti wa mwisho wa mapato na matumizi ya kaya uliofanyika Zanzibar mwaka 2014/15 ulionyesha kuwa kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi kilipungua kufikia 30.4 kutoka asilimia 34.9 mwaka 2009/2010.

“Nichukue fursa hii kuwasisitiza kuwa ni lazima muwe makini kuhakikisha kila taarifa mtakayoikusanya katika kaya inakuwa na ubora unaokubalika,”alisema.

Hata hivyo, aliwaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano wao wakati wa zoezi zima la kukusanya taarifa za utafiti huo kwani kufanya hivyo kutaiwezesha serikali kupata takwimu sahihi zitakazopima mabadiliko ya umaskini na kutathimini mafanikio katika maeneo mengine ya kiuchumi na kijamii.

Aliwahakikishia wananchi kuwa taarifa zitakazokusanywa zitatunzwa kwa siri  kubwa na zitatumika kwa shughuli za kitakwimu pekee.

Alisema kutoa takwimu sahihi ni wajibu wa kila mwananchi na kukataa au kutoa takwimu zisizo sahihi ni kwenda kinyume na sheria na adhabu yake ni faini au kifungo.

Mtakwimu Mkuu wa serikali, Mayasa Mahfoudh  alisema ubora wa takwimu ni muhimu iwapo kutakua na takwimu sahihi na kwa wakati, ambazo zitakidhi mahitaji.

Aliwataka wadadisi hao kujitahidi kufanya kazi kwa usahihi kwa kufuata mafunzo waliyopatiwa na wakufunzi wao.

Aliziomba serikali za mikoa kutoa ushirikiano kwa wadadisi hao ili kufanikisha zoezi hilo ambalo limegharimu fedha nyingi za serikali na washirika wa maendeleo.

Naye Mdhamini wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa serikali Pemba, Haroub Ali Massoud, alisema kuwepo kwa taarifa sahihi zitaisaidia serikali katika kupanga matumizi yake kwa ajili ya mipango ya maendeleo.

Naye  Mwenyekiti wa Bodi ya Takwimu Zanzibar, Dk. Said Gharib Bilal, aliwataka wadadisi kufanya kazi vizuri ili kuleta ufanisi na kuwaomba wananchi kushukuru kuwa kazi hizo zinafanywa na wazalendo wenyewe.

Utafiti huo utafanyika kwa ushirikiano baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, UNDP, UNWOMAN na UNICEF.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!