Wafanyakazi ZECO wapewa elimu ya UKIMWI

MWENYEKITI wa bodi ya wakurugenzi wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Shafi Mussa Haji, amezitaka taasisi na sekta mbalimbali nchini kushirikiana ipasavyo katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI ili kupunguza na kuondosha maambukizi mapya ya ugonjwa huo.

Akifungua mafunzo katika ukumbi wa Dk. Hanuni uliyopo Kidongochekundu, alisema ushirikiano katika sekta mbalimbali juu ya suala hilo itakuwa chachu ya kuwafikia wananchi wengi kujua athari na njia za kujikinga na maradhi hayo.

Alisema hatua hiyo itasaidia kueneza elimu juu ya suala hilo katika jamii na kuweza kuepukana maradhi hayo.

Sambamba na hayo alisema ni vyema kukatolewa elimu ya kutosha kwa wananchi ili kupata uelewa wa kina juu ya suala hilo ili kuepusha kutokea kwa athari zitakazopelekea kupoteza nguvu kazi ya jamii.

Mratibu wa taasisi ya wafanyabiashara wanaopambana na maradhi ya UKIMWI katika sehemu za kazi (ABCZ), Taalib Ussi Hamad, alitumia fursa hiyo kuzisisitiza sekta za kazi kuwa wawakilishi wazuri katika kuihamasisha jamii ili lengo la kutoa elimu katika sehemu za kazi iweze kufanikiwa.

Akiwasilisha mada ya mazingira hatarisha katika mafunzo hayo mkuu wa sera na mipango kutoka Tume ya UKIMWI, Halima Ali Mohammed, alisema ZECO inafika kila eneo na sehemu nyingi hivyo ni vyema kuwa na tahadhari ili kujiepusha na athari za maambukizo ambazo zitaweza kutokezea.

Washiriki wa mafunzo hayo ambao ni kutoka Shirika la Umeme Zanziba (ZECO), walisema kuna mazingira mbalimbali katika sehemu za kazi ambayo yanachangia kwa namna moja au nyengine kuweza kupata maambukizo hayo.

Hata hivyo, walieleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kuona namna gani wataweza kujikinga na kuepukana na maradhi hayo.

Mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na ZECO kwa kushirikiana na tume ya UKIMWI Zanzibar.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!