UN yaitaka dunia isitishe uhusiano wa kifedha na jeshi la Myanmar

Timu ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa imezitaka nchi za dunia kusitisha miamala ya kifedha na jeshi la Myanmar linaloendelea kuua Waislamu wa jamii ya Rohingya katika mkoa wa Rakhine.

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wametoa mwito huo leo Jumanne na kuongeza kuwa, katika uchunguzi wao hawakuona iwapo kuna ushahidi au jitihada zozote zinazofanywa na serikali ya Myanmar kwa ajili ya kuwapokea wakimbizi Warohingya.

Kadhalika timu hiyo ya uchunguzi ya UN kwa mara nyingine imetoa mwito wa kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria majenerali wa jeshi la Myanmar waliohusika katika jinai dhidi ya Waislamu Warohingya.

Christopher Sidoti, mmoja wa waatalamu hao wa UN ambaye ni wakili wa haki za binadamu raia wa Australia amesema, “Kutokana na uzito wa jinai za nyuma na za sasa, kuna haja ya kukatwa miamala ya kifedha, kisiasa na kiuchumi na jeshi la Myanmar ili tuweze kuwatambua wahusika halisi wa jinai hizo.”

Siku chache zilizopita, jeshi hilo la Myanmar liliendelea kufanya jinai dhidi ya Waislamu huko magharibi mwa nchi hiyo ambapo katika jinai mpya liliwamiminia risasi makumi ya Waislamu hao, ambapo sita miongoni mwao waliuawa huku wengine wanaokaribia 300 wakitiwa mbaroni.

Wanajeshi katili wa Myanmar

Itakumbukwa kuwa, jeshi hilo kwa kushirikiana na Mabudha wenye misimamo ya kigaidi lilifanya mauaji makubwa dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya, miaka miwili iliyopita katika jimbo hilo la Rakhine.

Katika hujuma hizo jeshi hilo liliua karibu Waislamu elfu saba wa jamii ya Rohingya na kuwajeruhiwa wengine elfu nane, huku wengine zaidi ya milioni moja wakilazimika kuwa wakimbizi nje ya nchi hiyo.

error: Content is protected !!