UN: Raia 8,000 wa Afghanistan wameuawa, kujeruhiwa 2018

Ripoti mpya ya Ujumbe wa Usaidizi wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan (UNAMA) imesema raia zaidi ya elfu nane wa Kiafghani wameuawa na kujeruhiwa katika kipindi cha miezi tisa ya kwanza ya mwaka huu 2018.

Ripoti ya UNAMA iliyotolewa jana Jumatano imesema kuwa, kumeshuhudiwa ongezeko la asilimia 5 ya vifo vya raia nchini humo mwaka huu, ikilinganishwa na mwaka jana.

UNAMA imesema idadi ya raia waliouawa nchini humo tangu mwaka huu uanze hadi mwezi uliopita wa Septemba ni 2,798, huku wengine 5,252 wakijeruhiwa.

Tadamichi Yamamoto, ofisa wa ngazi za juu wa UN nchini Afghanistan amesema kuwa, uingiliaji wa kijeshi nchini Afghanistan ndani ya miaka 17 umekosa kuzaa matunda, hivyo basi Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena unatoa mwito wa kupatiwa ufumbuzi mgogoro uliopo kwa njia za amani haraka iwezekanavyo.

Askari wa US nchini Afghanistan

Taasisi moja isiyo ya kiserikali inayoijulikana kwa jina la “Kundi la Kupigania Usalama wa Raia Afghanistan” imesema katika ripoti yake ya hivi karibuni kabisa kuwa, zaidi ya raia mia moja wameuliwa kwenye mashambulizi ya anga ya Marekani na NATO katika mikoa 12 ya Afghanistan kwenye kipindi cha mwezi Septemba mwaka huu 2018 pekee.

Mwaka 2001, Marekani ilituma wanajeshi wake kwenda kuivamia Afghanistan kwa madai ya kupambana na ugaidi, kuleta amani ya kudumu na kuwaandalia mazingira na maisha bora wananchi wa Afghanistan.

error: Content is protected !!