UN: Hali ya wahajiri nchini Libya inatia wasiwasi sana

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa hali ya wahajiri nchini Libya inatia wasiwasi mkubwa.

Katika ripoti yake kwa Umoja wa Mataifa, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa umoja huo amesema kuwa, hivi sasa kuna zaidi ya wahajiri haramu 3,400 wamekwama nchini Libya na wanaishi katika mazingira magumu sana.

Amesema, wahajiri wanaoshikiliwa katika korokoro ya Zintan wana matatizo chungu nzima ikiwemo lishe dunia na njaa kali. Ameongeza kuwa, kila mkimbizi aliyeko kwenye korokoro hiyo huwa anapewa kipande cha mkate mkavu chenye uzito wa gramu 200 tu kwa siku.

Ripoti ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, tangu mwezi Septemba 2018 hadi hivi sasa, wahajiri 22 wamepoteza maisha yao kutokana na ugonjwa wa kifua kikuu na maradhi mengine hatari yakiwemo ya kuambukiza.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, raia 432 wa Eritrea wakiwemo watoto wadogo 132 ambapo zaidi ya 60 kati yao wamekumbwa na ugonjwa wa kifua kikuu, wanashikiliwa katika korokoro ya Zintan huko Libya.

Raia wengi wa nchi za Afrika wanaokimbia machafuko na umaskini unaotokana na siasa za kibeberu za madola ya Magharibi, huwa wanajitumbukiza kwenye majanga mazito kama hayo kwa tamaa ya kuelekea barani Ulaya. 

Asilimia kubwa ya wahajiri hao haramu huwa hawafiki wanakokwenda, kwani imma hupoteza maisha kwa kuzama baharini, au hupigwa mnada kama bidhaa sokoni, au huingia mikononi mwa megenge ya magendo ya binadamu au huishia jela.

error: Content is protected !!