Ukweli kuhusu mgomo wa wafanyakazi kitengo cha huduma kwa wateja Zantel, Zanzibar

Wafanyakazi wa shirika la mawasiliano ya simu Zanzibar Telecom Limited (ZANTEL) kitengo cha huduma kwa wateja wamegoma kufanya kazi hiyo kwa madai kuwa mshahara wanaolipwa na shirika hilo ni mdogo na utaratibu wa kazi hauzingatii usalama wa afya ya mfanyakazi.

Mgomo huo umefanyika mapema jana Septemba 28 majira ya asubuhi nje ya ofisi za ZANTEL Amani Mjini Unguja.

Wafanyakazi kitengo cha huduma kwa wateja Zantel wagoma kuingia sehemu yao ya kazi

Wafanyakazi hao ambao ni Wanafunzi waliomaliza Digree na Diploma za fani tofauti kutoka chuo cha Zanzibar University (ZU) na chuo cha Karume Institute of Science and Technology (KIST) wamelalamikia mazingira ya kazi kuwa si salama kwa afya zao na mshahara wanaopewa haukidhi mahitaji.

Wamesema wanafanya kazi kwa saa 8 kila siku na kwa mtu mmoja hupokea zaidi ya simu 160 hadi 200 kwa siku jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.

Maimuna Moh’d ni mmoja miongoni mwa wanaoshiriki mgomo huo amelalamikia mazingira ya kazi kuwa si salama kwa afya zao kwani wapo miongoni mwao walioathirika masikio, meno na uti wa mgongo ambapo shirika halikuwa na msaada wowote kwa wenzao waliopatwa na maradhi.

“Tunafanya kazi katika eneo lililojaa umeme na komputa nyingi zilizoachwa wazi saa 24 kuhakikisha wanaowasiliana na kitengo cha huduma kwa mteja wanapata huduma saa zote, mbaya zaidi ndani ya chumba hicho kuna baridi ya hatari kama tupo kwenye friji”, na mwisho wa mwezi binafsi napewa mshahara laki mbili tu hainikidhi hata kuangalia afya yangu” Amesema Maimuna.

Ni utaratibu uliyopo kwa takribani miaka 4 sasa wanafunzi wanaosomea fani tofauti kutoka chuo cha ZU na KIST baada ya kuhitimu masomo yao hupelekwa kufanya kazi ZANTEL kwa muda wa miezi 18 kwa dhumuni la kujijengea uzoefu wa ufanyaji kazi.

Kwamujibu wa Afisa mkuu wa mipango tawala na rasilimali watu wa Chuo cha Karume (KIST) Bakari Hamza Haji amesema Utaratibu huo upo kisheria baada ya vyuo hivyo kufunga mkataba na shirika la ZANTEL ambapo walikubaliana Wanafunzi hao walipwe kiasi cha Tsh. 1800 kwa kila saa watakalofanyia kazi.

Wanafunzi hao wamesema binafsi hawajauona mkataba uliofungwa baina ya vyuo walivyotoka na shirika la ZANTEL huku wakisema tangu wafike kufanya kazi hakukuwa na ushirikiano wowote baina yao na wahusika kutoka vyuoni kwao.

Afisa tawala wa chuo cha KIST amesema mkataba unasema wanafunzi hao hawakupelekwa ZANTEL kama wafanyakazi bali ni wanafunzi “Chuo kiliomba kuwapeleka wanafunzi pindi wakimaliza masomo kama Graduate Scientisty na si wafanyakazi kwa sharti la kuhudumu kwa miezi 18 na mkataba huo ulifungwa baina ya chuo na ZANTEL mwaka 2015-2016”.

Amesema wao kama chuo wamepokea malalamiko hayo na wapo katika mchakato wa kuzungumza na ZANTEL ili kutafuta muafaka juu ya suala hilo“Siku ya Jumatano walileta malalamiko yao hapa chuoni kuwa posho ya 1800 kwa saa ni ndogo hivyo wanahitaji waongezewe iwe 3500 kwa saa lakini tukiwa katika utaratibu wa kutafuta suluhu juu ya suala hilo  tumeshangazwa leo wanafunzi wetu kugoma kabisa kufanya kazi huko”

Nusu ya wanafunzi hao hawajashiriki mgomo huo na wanaendelea kufanyakazi.

Waandishi wa habari hizi wamejitahidi kumtafuta HR wa shirika la ZANTEL ili kumsikia nae anayepi ya kusema juu ya mgomo huo wa wafanyakazi lakini jitihada hizo zimegonga mwamba ambapo mmoja kati ya wasimamizi wa shirika hilo amesema HR hayupo kazini kutokana na hali yake kutokuwa nzuri kiafya.

error: Content is protected !!