Tumieni wataalamu wastaafu kupata ufanisi

Sekta ya afya inaweza kupiga hatua kubwa za maendeleo hasa katika nchi zinazoendelea iwapo wataalamu wazoefu wastaafu wataendelea kutumika na kutumia uzoefu wao kwa faida ya jamii.

Profesa Li Rongshan, Mtendaji Mkuu katika Hospitali ya jimbo la Shanxi alisema serikali katika nchi nyingi zinazoendelea zimeshindwa kuwatumia wataalamu wazoefu wa afya katika nchi zao hali inayopelekea sekta ya afya kukumbwa na changamoto nyingi katika nchi hizo.

Akizungumza na watendaji wa sekta ya afya kutoka Zanzibar katika ukumbi wa Shanxi Jingmao, alisema sio vyema kuwaachia wataalamu wa afya wazoefu wakiodoka katika utendaji kwa kisingizio cha umri wa kumaliza muda wa utumishi wakati taaluma na uzoefu wao bado vinaweza kuwabakisha katika utendaji.

“Changamoto zetu za sekta ya afya ni nyingi hasa katika nchi zinazoendelea, wataalamu wetu wazoefu tunao lakini tunashindwa kuwatumia kwa kisingizio cha kutiiza umri wa kustaafu,” alisema na kuongeza kuwa licha ya watendaji hao wazoefu kumaliza umri wa utumishi lakini pia wanaweza kutumika kama washauri katika sehemu walizotokea.

Alisema kinachogomba na kutia hofu zaidi ni mvutiano wa madaraka (conflict of interest) kwa watendaji vijana kuona wanashindwa kupata nafasi na wazoefu wakidhani kuwa wanaweza kubakia katika nafasi hizo kwa muda mrefu hata baada ya muda wa kustaafu.

Alisema katika kufanikisha suala hili lazima kuwepo na mgawanyo wa kiutendaji kwa kuwapangia wataalamu wazoefu wastaafu katika sehemu za ushauri na utatuzi wa changamoto zinazoshindwa kupatiwa ufumbuzi na watendaji wataalamu vijana.

“Sekta ya afya ina changamoto nyingi sana, kila siku linazuka jambo jengine ambalo linahitaji utatuzi, watumieni wataalamu wazoefu, uzoefu wao ni muhimu katika sekta ya afya,” alisema na kuongeza kuwa wengi wanaoondoka katika utumishi bado wana kuwa na nguvu na uwezo wa kufanya kazi.

Profesa Li alisema inachukua muda mrefu na matumizi ya fedha na rasilimali nyingi hadi kuweza kumpata mtaalamu-stahiki katika sekta ya afya lakini matumizi yake yanakuwa ya muda mfupi tu kutokana na umri tunaojipangia katika utumishi.

Alisema eneo jengine muhimu la kuweza kuwatumia wataalamu hao wazoefu ni katika taaluma kwa kuwaandaa vijana katika sekta mbali mbali ili waje kutumika katika nafasi zao wanapoamua kundoka katika utumishi wa kitaalamu.

“Wataalamu hawa wanasomeshwa na kufunzwa kwa kutumia fedha nyingi ambazo hata zingelifaa kutumika katika sehemu nyengine za msingi, lakini tunawekeza katika taaluma ili waje kufanya kazi ya kusaidia jamii ikiwemo kwenye sekta ya afya watumike katika kugundua na kutibu magonjwa lakini tunawaacha katima muda mfupi tu wa utumishi wao, wengi wao wakiwa bado wanahitajika” alisema na kuongeza kuwa, “mataifa ya magharibi yanawatunza na kuwathamini sana wataalamu wazoefu hata wanapofikia muda wa kustaafu.”

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!