Trump atishia kulipigia kura ya veto azimio la Kongresi dhidi ya Saudia

Rais Donald Trump wa Marekani ametishia kupiga kura ya veto dhidi ya azimio lolote la Kongresi ya nchi hiyo linaloitaka serikali yake kukomesha misaada ya kijeshi kwa muungano wa Saudi Arabia katika vita dhidi ya taifa la Yemen.

Ripoti zinasema kuwa, Donald Trump ametishia kwamba ataupinga kwa kura ya veto uamuzi wowote unaozuia misaada ya kijeshi kwa Saudi Arabia na washirika wake katika vita vya Yemen kwa madai kwamba azimio kama hilo linavuruga uhusiano wa Marekani na nchi za Mashariki ya Kati na kutia doa juhudi za serikali ya Washington za eti “kupambana na ukatili na misimamo mikali”.

Uamuzi huo wa Trump umechukuliwa wiki mbili baada ya wawakishi wa Kongresi ya Marekani kutoka vyama vyote viwili vya Republican na Democratic kuwasilisha muswada unaohusiana na misaada ya kivita ya serikali ya Donald Trump. Muswada huo uliwasilishwa na wabunge wa Marekani wakipinga jinai zinazofanywa na Saudi Arabia  huko Yemen na mauaji ya utawala wa kifalme wa nchi hiyo dhidi ya mwandishi na mkosoaji wa serikali ya Riyadh, Jamal Khashoggi. 

Ijumaa iliyopita Donald Trump alipuuza muhula wa mwisho iliokuwa umetolewa na Kongresi iliyomtaka kubaini nani aliamuru mauaji ya mwandishi habari na mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi na iwapo ataiwekea vikwazo Saudi Arabia au la. Suala hilo limewakasirisha sana wabunge wa Marekani.

Jamal Khashoggi, aliyewahi kuwa msiri na mwandani wa aila ya kifalme inayotawala nchini Saudi Arabia, lakini hatimaye akageuka kuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal Saud, aliuliwa na mwili wake kukatwa vipande vipande, alipoingia kwenye jengo la ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki mnamo tarehe Pili Oktoba ili kukabidhi hati zake kwa ajili ya mpango wake wa kufunga ndoa.     

error: Content is protected !!