Timu ya 29 madaktari wa Kichina yaanza kazi Abdalla Mzee

TIMU ya 28 ya madaktari kutoka China waliokuwa wakifanya kazi katika hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani,wameagwa baada ya kumaliza muda wao wa kazi uliodumu kwa mwaka mmoja.

Nafasi yao imechukuliwa na madaktari wengine wa timu ya watu 29.

Akiwaaga madaktari hao, Ofisa Mdhamini Wizara ya Afya Pemba, Shadya Shaaban Seif, aliipongeza China kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo afya.

Alisema katika kipindi chao cha kuhudumu kulikuwa na mabadiliko makubwa ya utoaji huduma na kwamba wananchi walifarajika na huduma walizopata.

Aidha alisema, tayari hospitali hiyo imepokea madaktari mbadala ambao wataziba pengo lao.

Akizungumzia mafanikio,alisema  ni kutoa tiba bora za upasuaji na kuendesha mafunzo kwa kutibu maradhi mbali mbali kwa madaktari wazalendo.

Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Haji Mwita Haji,alisema timu iliyopita imejitahidi kutoa huduma bora kwa wananchi na matarajio yake madaktari wanaokuja kuziba nafasi zao, wataendelea kufuata nyayo za watangulizi wao.

Kwa upande wake kiongozi wa madaktari hao, Cao Wei, alisema walipata ushirikiano mzuri kutoka kwa madaktari na serikali licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo baadhi ya vifaa kutofanya kazi.

“Kuharibika kwa baadhi ya vifaa ikiwemo CT Scan ilisababisha usumbufu mkubwa katika kutoa huduma kwa jamii, lakini tulijitahidi,” alisema.

Aliiomba serikali kufanya juhudi kuharakisha kutengeneza mashine hiyo ili madaktari waliokuja waweze kuendelea kutoa huduma katika mazingira mazuri.

“Naiomba serikali kufanya matengenezo ya mashine hii ili iweze kutoa huduma bora kwa wagonjwa wanaofika hospitalini hapo kwa matibabu,” alisema.

Kiongozi wa timu ya watu 29 ya madaktari hao, Dk. Yuan, aliomba ushirikiano kutoka kwa wafanyakazi wa hospitali hiyo ili kuifanya kazi yao iwe nyepesi.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!