Taasisi za SMZ zapewa mafunzo ya Upishi, ukarimu

 

TAASISI mbalimbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Taasisi binafsi, zimepata fursa ya kushiriki katika mafunzo ya awamu ya pili ya mapishi na Ukarimu, ambayo yameanza rasmi Septemba 9 na kumalizika Septemba 29 mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Haji Issa Gavu wakati alipokuwa akifungua mafunzo hayo katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Alisema, mafunzo hayo yameandaliwa na Taasisi ya vyakula na huduma ya Taifa ya China, na yalianza mwaka jana ambapo yalijumuisha washiriki 30 na kwa mwaka huu walioshiriki ni 50.

Aidha Waziri Gavu alisema, lengo la kuanzishwa kwa mafunzo hayo ni, kuwawezesha washiriki kutoa huduma bora zaidi za ukarimu, ambazo zinawavutia wageni hasa watalii na wakuu wa nchi wanaokuja kutembelea nchini hapa.

“Mkipata ujuzi na mbinu bora zaidi za kutoa huduma za ukarimu, zitawavutia wakuu wa nchi wageni na wale wote ambao watakuwa wanakuja kuitembelea Zanzibar  kwa namna moja au nyengine” Aliongeza.

Aliongeza na kusema kuwa, mafunzo hayo yameendelezwa kutokana na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein, wakati alipozungumza na Balozi mdogo wa China kwa kumuomba kwamba ni vyema na ni busara jambo hilo kuwa ni endelevu.

 

 

 

CHANZO: ZANZIBAR LEO

 

error: Content is protected !!