Taa za kuongozea gari Chake Chake zapata hitilafu

TAA za kwanza za kuongozea gari kisiwani Pemba, zilizofungwa katika mji wa Chake Chake, zimepata hitilafu muda mfupi tokea zianze kutoa huduma.

Hali hiyo imewafanya madereva kurudi katika mfumo wao wa zamani wa utumiaji wa barabara.

Taa hizo zilipata hitilafu kabla ya sikukuu ya Eid El Fitri, takribani muda usiozidi wiki moja tokea zifungwe.

Ofisa Mdhamini Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Pemba, Hamad Ahmed Baucha, alikiri kuwepo tatizo hilo na kuwataka watumiaji wa barabara kuwa na subira.

Alisema kwa kuwa serikali imeamua kuweka taa hizo, tatizo lililojitokeza litashughulikiwa na taa hizo zitafanya kazi kama kawaida.

Alieleza ofisi yake imeshafanya mawasiliano na kampuni iliyopewa kazi ya kufunga taa hizo.

“Sisi tayari tumeshazungumza na wenzetu waliopewa kazi hili, watakuja muda wowote kuweka sawa, naamini tatizo lililojitokeza la taa kutofanya kazi litaondoka,” alisema.

Alisema kwa sasa bado taa hizo hazijakabidhiwa serikalini kwani bado ziko chini ya uangalizi wa kampuni ya TASEME ambayo ndio iliyozifunga.

“Baada ya kuwaeleza hali halisi ya tatizo hili, wao waliniahidi kuwa taa hizo zitafanya kazi kama kawaida, lakini mpaka sasa bado hazijafanya kazi tena na wamesema watakuja kuangalia tatizo,” alieleza.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!