Sisitizo la kuendeleza mazungumzo ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa Venezuela

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ametilia mkozo azma ya serikali yake ya kuendeleza mazungumzo na wapinzani chini ya uwenyeji wa Norway.

Maduro ameunga mkono kuanzishwa meza ya mazungumzo ya kudumu ili kupata njia ya ufumbuzi na kufikia mapatano ya kumaliza hitilafu za kisiasa kati ya wawakilishi wa serikali na wapinzani; na kusisitiza kuwa katika mwaka huu wa 2019 atafikia mapatano makubwa kuhusu amani ya Venezuela.  

Baada ya kugonga mwamba saisa za mabavu na vitisho; na vile vile wapinzani kuendesha njama kubwa pamoja na waungaji mkono wao ili kutekeleza njama ya mapinduzi na wakati huo huo kuongeza mashinikizo ya kisiasa na kijamii dhdi ya serikali ya Maduro; hivi sasa duru mpya ya jitihada za kieneo na kimataifa imeanza kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Venezuela kupitia mazungumzo. Kuhusiana na suala hilo, tangu siku kadhaa zilizopita kumefanyika duru mbili za mazungumzo kati ya wawakilishi wa serikali ya Venezuela na wapinzani huko Oslo. Katika mazungumzo hayo kulizingatiwa suala la kufikia mapatano ili kujinasua katika mkwamo wa kisiasa wa sasa nchini humo. Hata hivyo ukwamishaji wa wapinzani wanaoungwa mkono na Marekani umeyapeleka mrama mazungumzo hayo, kufuatia tangazo lao kuwa hawatashiriki tena mazungumzo hayo. Wapinzani wanataka tu Maduro ang’atuke madarakani na uchaguzi mpya ufanyike nchini. 

Pamoja na hayo yote, juhudi za kimataifa za kuendesha duru mpya ya mazunguzo zingali zinaendelea. Duru hiyo mpya ya mazungumzo inatazamiwa kufanyika huko Oslo ili kupata ufumbuzi wa mgogoro wa Venezuela. Wakati huo huo Peru pia imetoa pendekezo la kufanyika mkutano mpya katika jitihada hizo hizo za kutafuta njia zinazofaa za kuhitimisha mgogoro wa Venezuela. Mkutano huo unatazamiwa kuhudhuriwa na nchi kadhaa muhimu.  

Katika hali ambayo juhudi mbalimbali zinaendelea kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro wa Venezuela kupitia njia za kisiasa; Marekani kwa upande wake inaendeleza uhasama wake na kuingilia masuala ya ndani ya Venezuela kwa kumuunga mkono Juan Guaido kiongozi wa upinzani nchini humo. Kama ilivyoshuhudiwa juzi Ijumaa ambapo Mike Pompeo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani alitoa taarifa ya kumpongeza kiongozi huyo wa upinzani kwa mnasaba wa maadhimisho ya uhuru wa nchi hiyo. 

Wapinzani wa Maduro ndani ya nchi wamegawanyika licha ya uungaji mkono wote wanaopata kutoka Washington. Ukweli wa mambo ni kuwa Guaido ameshindwa kuimarisha nafasi yake kama kiongozi wa wapinzani nchini Venezuela kutokana na kutokuwa na uungaji ho mkono mkubwa wa wananchi na vile vile kutii kwake kikamilifu maamrisho ya kisiasa ya Washington. Kama ilivyoshuhudiwa wazi wiki iliyopita ambapo wananchi walilalamika vikali kuhusiana na msimamo wake huo na hivyo kumlazimika kufutilia mbali hotuba aliyopanga kuitoa. Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa tangu Aprili 30 mwaka huu ambapo jaribio la wapinzani la kutaka kumpindua Maduro lilifeli, harakati za wapinzani zimepungua, idadi ya watu wanaoshiriki katika mikutano yake kupungua na wapinzani hawajafanya maandamano yoyote makubwa.  

Diosdado Cabello Spika wa bunge la Waasisi la Venezuela ameashiria namna Guaido kiongozi wa wapinzani Venezuela alivyo tatizo kwa upande wa upinzani na waungaji mkono wao huko Marekani na kueleza kuwa kila kunapofanyika juhudi za kufanyika mazungumzo, wapinzani ndio wanaotoka kwenye meza ya mazungumzo kwa sababu hawawezi kufikia mapatano baina yao. 

Kwa kuzingatia kuongezeka juhudi za kimataifa za kufanikisha mazungumzo na kufikiwa mapatano ya kisiasa ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Venezuela, sasa wapinzani hawana tena budi ila kuchukua uamuzi wa msingi wa ima kufanya mazungumzo na kuheshimu sheria au kuendelea kuvunja sheria na hivyo kuendeleza mgogoro wa nchi hiyo. 

error: Content is protected !!