Serikali yapata hasara ya 250m/- kuvuja kwa mitihani

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma, amesema mtu yeyote ambae atabainika kuhusika na uvujishaji wa mitihani, atachukuliwa hatua.

Aliyasema hayo katika ukumbi wa elimu mbadala Rahaleo, wakati akizungumza na watendaji wa baraza la mitihani Zanzibar.

Alisema sababu ya kukutana na watendaji hao ni kutokana na kuonekana kushindwa kusimamia vyema mitihani ya kidato cha pili na kusababisha kuvuja.

Alisema tukio la kuvuja mitihani limeisababishia hasara kubwa serikali ambapo zaidi ya shilingi milioni 250 zimepoteza.

Alisema mbali na kutia hasara serikali imesababisha hasara kwa wazee na wanafunzi.

“Mtihani ni roho ya nchi endapo tutaivujisha tutakuwa na taifa legelege ambalo litashindwa kuzalisha wataalamu hapo baadae,” alisema.

Alifahamisha kuwa taarifa za uvujaji wa mitihani hiyo zilitoka kwa raia mwema na kueleza kuwa baadhi ya watu waliuza mitihani kwa shilingi 20,000.

Hata hivyo, alisema suala hilo linaendelea kufanyiwa kazi na vyombo vya ulinzi na usalama.

Naibu Waziri wa hiyo, Mmanga Mjengo Mjrawiri, alisema kitendo kilichofanyika ni cha upungufu wa maadili, hivyo wizara haitokuwa tayari kutiwa dosari na watu wachache.

Mkurugenzi wa Baraza la Mitihani, Zubeir Juma Khamis, alisema bado hawajui sehemu ambayo mitihani hiyo ilivuja lakini aliahidi kwamba hatua zitachukuliwa kuhakikisha mitihani ya marudio inafanywa katika mazingira salama.

 

 

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!