Serikali kusaka misumeno ya moto nyumba kwa nyumba

WIZARA ya Kilimo, Maliasili Mifugo na Uvuvi, Zanzibar, inakusudua kuendesha msako wa nyumba kwa nyumba, ili kukamta misumeno ya moto, ikiwa ni hatua ya kupunguza vitendo vya ukataji miti ovyo.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Makame Ali Ussi, alisema hayo Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar, wakati akijibu suala la  Mwakilishi wa jimbo la Kijitoupele, Ali Suleiman Shihata, aliyetaka kujua Zanzibar imejaaliwa kuwa na Minazi mingi, lakini kwa bahati mbaya sana imekatwa kwa ajili ya kufanyiwa mbao za milango madirisha.

Akijibu suala hilo Naibu huyo alisema, kumekuwa na hali mbaya ya ukataji wa miti unaoendelea kufanyika kutokana na kuwapo kwa misumeno ya moto jamba ambalo limesababisha kuwepo kwa upungufu wa   minazi kwa upande wa Zanzibar kutokana na miti hiyo kutumika  kwa shughuli za kijamii.

Kutokana na hali hiyo, Naibu huyo, alisema Wizara hiyo hivi sasa imepanga kuendesha operesheni ya nyumba kwa nyumba, ili kuweza kudhibiti misumeno hiyo, kwa vile hali ya zao la minazi  hivi sasa imekuwa mbaya kwa Zanzibar.

Alisema kwa mujibu wa sensa ya miti ya mwaka 2013 (Woody Biosmass Survey) imeonesha  kutoka mwaka 1997 hadi 2013 minazi imepungua kutoka 3,317,600.00 hadi 1,255,000.00 kwa Unguja na Pemba kutoka 1,888,000 hadi 1,044,000.00

Alisema hali hiyo inatisha kwani kiwango cha upunguaji minanzi kinaathiri sekta ya nyingi ikiwemo uchumi wa  Nchi.

Alisema Wizara hiyo, kwa kuzingatia suala la bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019, ilijipanga kuotesha jumla ya miche ya minazi 200,000, lakini imeweza kuotesha miche 86,631 Unguja 61,631 na Pemba 25,000.

Aidha, alisema katika vitalu vya serikali kwa lengo la kuitoa kwa wakulima bila ya malipo, ili kurejesha miti ambayo ina umuhimu mkubwa wa kiuchumi na kijamii kwa hapa Zanzibar.

Alisema wamekuwa wakiendesha sensa ya miti kila baada ya miaka mitatu ikiwa ni hatua inayoisaidia serikali kutambua idadi ya miti iliyonayo hapa nchini.

Alisema katika utafiti uliofanywa na Wizara hiyo, imebaini minazi mirefu  ndio bora Zaidi kwa vile ina uwezo wa kukaa kwa muda mrefu na kuzalisha nazi kwa wingi.

Kuhusu suala la kuweka adhabu ya papo kwa papo kwa watu wanaokata minazi bila ya kibali, alisema suala hilo limekuwa likifanyiwa kazi lakini baadhi ya kesi huhitaji kufika katika ngazi ya Mahakama.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!