Seneta Ghraham: Kukana kwamba Bin Salman aliamuru kuuawa Khashoggi ni kujifanya kipofu

Seneta mashuhuri wa Marekani Lindsey Graham amekosoa vikali siasa za Saudi Arabia na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa nchi hiyo Muhammad bin Salman na kusisitiza kuwa, Kongresi ya Marekani itachukua msimamo mkali ili kukomesha sera mbovu za Riyadh bila ya kujali msimamo wa serikali ya Rais Donald Trump.

Lindsey Graham amesema kwamba, mauaji yaliyofanywa na utawala wa Saudi Arabia dhidi ya mwandishi na mkosoaji wa nchi hiyo, Jamal Khashoggi, mashambulizi na uvamizi wa nchi hiyo huko Yemen, kuizingira Qatar na jaribio la Saudia la kutaka kumuondoa madarakani Waziri Mkuu wa Lebanon, Saad al Hariri yote hayo ni kielelezo cha sera za kijuba na ukiukaji wa sharia za kimataifa.

Seneta huyo mashuhuri ambaye anatajwa kuwa ni mtu wa karibu kwa Rais Donald Trump wa Marekani amesema hayo yote ni sehemu ya siasa za Riyadh zinazovuruga na kuteteresha amani Mashariki ya Kati.

Graham amekosoa pia siasa za serikali ya Marekani na hoja zinazotumiwa na Washington kwa ajili ya kutetea uhusiano wake na utawala wa Riyadh na kufumbia jicho matendo na mienendo ya Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman.

Amesema kitendo cha kukana kwamba Bin Salman alihusika na mauaji ya Jamal Khashoggi ni kujifanya kipofu kwa makusudi na ametahadharisha kwamba, kutomuadhibu Bin Salman kutatoa ujumbe mbaya na kuwaruhusu viongozi madikteta kuwamaliza wapinzani wao.

Jamal Khashoggi, aliyewahi kuwa msiri na mwandani wa familia ya kifalme inayotawala nchini Saudi Arabia, aligeuka na kuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal Saud. Jamal aliuliwa tarehe Pili Oktoba mwaka huu na timu ya mauaji iliyotumwa Istanbul Uturuki na Muhammad bin Salman baada ya kuingia kwenye jengo la ubalozi mdogo wa nchi hiyo na mwili wake ukakatwa vipande vipande.

error: Content is protected !!