Saudia yapinga takwa la Uturuki la kufanya uchunguzi wa mauaji ya Khashoggi kuwa wa kimataifa

Kufuatia mashinikizo ya kieneo na kimataifa ya kutaka kufuatiliwa kimataifa faili la mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari na mkosoaji wa utawala wa Aal-Saud, serikali ya Riyadh imekataa kuufanya wa kimataifa uchunguzi wa faili hilo.

Jumatano ya jana Rais Recep Tayyip Erdoğan alitangaza kwamba Ankara itaendelea kufuatilia faili la mauaji ya mwandishi huyo na kwamba iwapo itahitajika basi faili hilo litawasilishwa katika mahkama ya kimataifa. Kufuatia hali hiyo, Bandar bin Mohammed Al-Aiban, Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Saudia na katika kujaribu kuzuia kuendelea kufichuliwa zaidi kashfa za viongozi wa nchi hiyo, amekataa pendekezo hilo la kuufanya uchunguzi huo kuwa wa kimataifa. Kabla ya hapo pia kanali ya televisheni ya Al Jazeera ilifichua kwamba mwili wa Jamal Khashoggi, ambaye aliuawa na maafisa wa usalama wa Saudia na kwa amri ya Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalmbe wa nchi hiyo, uliteketezwa kwa moto katika tanuri lililojengwa katika makazi ya balozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul.

Khashoggi alitoweka katika mazingira ya kutatanisha baada ya kuingia katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki tarehe pili Oktoba mwaka jana. Hatimaye Saudia ililazimika kukiri tarehe 19 ya mwezi huo kwamba mwandishi huyo mkosoaji wa Riyadh aliuawa ndani ya ubalozi wake, kufuatia mashinikizo makali ya dunia, baada ya kuwa ilikadhibisha kwa mara kadhaa kuhusika kwa aina yoyote na jinai hiyo. Jamal Khashoggi alikuwa katika orodha ya watu waliokuwa wanafuatiliwa na utawala wa Saudia kwa ajili ya kukamatwa.

error: Content is protected !!