Pongezi kwa munasaba wa Maulid ya Mtume Mtukufu SAW wa Uislamu na kuanza Wiki ya Umoja

Leo Jumanne, 12 Rabiul Awwal mwaka 1440 Hijria Qamaria, sawa na Novemba 20 2018, kwa mujibu wa baadhi ya riwaya ni siku ya kukumbuka na kuadhimisha kuzaliwa (Maulid) Bwana Mtume Muhammad al Mustafa SAW, Mtume Mtukufu wa Uislamu. Siku hii pia ni mwanzo wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu.

Kwa mujibu wa riwaya za Ahul Sunna wal Jamaa, Mtume Muhammad SAW alizaliwa tarehe 12 Rabiul Awwal na kwa mujibu wa riwaya za Shia tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huohuo ndiyo siku aliyozaliwa Mtukufu huyo.

Kwa msingi huo, Imam Khomeini, MA, Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni wenye kunadi umoja wa ulimwengu wa Kiislamu, alitangaza kipindi cha wiki moja cha baina ya siku hizo mbili, yaani kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani. Wiki ya umoja imekuwa fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu. Umoja wa Waislamu ni muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho kuna kila aina ya fitina na machafuko.

Ingawa Waislamu wanafuata madhehebu mbali mbali, lakini nukta ambazo wanaafikiana ni za kimsingi na ni nyingi kuliko zile ambazo wanahitilafiana. Kwa mfano Waislamu wote wanaafikiana kuhusu kumuamini Mungu Mmoja, kitabu kimoja yaani Qur’ani Tukufu, Mtume SAW na Kibla kimoja. Aidha Waislamu wanaafikiana kuhusu kutekeleza ibada muhimu kama vile Sala, Hija na pia kutoa Zaka n.k.

error: Content is protected !!