Pelosi: Kufukuzwa kwa Jeff Sessions kutazusha mgogoro wa kikatiba Marekani

Kiongozi wa wabunge wa chama cha Democratic katika Kongresi ya Marekani amesema kuwa kufukuzwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Jeff Sessions ni katika jitihada za Rais Donald Trump za kutaka kudhoofisha na hatimaye kukomesha uchunguzi wa kuingilia Russia uchaguzi uliomfikisha madarakani Trump mwaka 2016.

Nancy Pelosi aliyasema hayo jana baada ya Trump kumlazimisha Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Jeff Sessions kujiuzulu na kuongeza kuwa: Kaimu wake Matthew Whitaker pia anapaswa kuacha uchunguzi kuhusu faili la Russia katika uchaguzi wa rais uliopita.

Kiongozi wa Wademokrat katika Kongresi ya Marekani amesema kuwa, iwapo kujiuzulu kwa Jeff Sessions ni sehemu ya maandalizi ya kukomeshwa uchunguzi wa mkaguzi wa faili la Russia, Robert Mueller basi suala hilo litazusha mgogoro wa kikatiba nchini Marekani.

Mbunge Jerry Nadler pia amesema Trump anapaswa kusailiwa baada ya kumfukuza kazi Mwanasheria Mkuu Jeff Sessions.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa Sessions alikuwa akiunga mkono uchunguzi unaofanywa na Robert Mueller kuhusu madai ya ushirikiano uliokuwepo baina ya Russia na timu ya uchaguzi ya Donald Trump katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2016. Matthew G. Whitaker aliyeteuliwa na Trump kukaimu nafasi hiyo alikuwa miongoni mwa wapinzani wakubwa wa uchunguzi huo.

Baada ya chama cha Demokratic kushinda uchaguzi wa katikati ya muhula uliofanyika Novemba 6 na kujinyakulia viti vingi vya Baraza la Wawakilishi, kuna uwezekano kwamba, Kongresi inaweza kuzidisha kasi uchunguzi kuhusu faili la ushirikiano wa timu ya Trump na Russia katika uchaguzi uliopita wa rais.

error: Content is protected !!