Onyo la Rais Rodrigo Duterte wa Ufilipino kwa Marekani kuhusiana na siasa zake dhidi ya China

Rais Rodrigo Duterte wa Ufilipino amekiri kwamba Marekani inaiwekea mashinikizo nchi yake ili isimame imara kukabiliana na China kuhusiana na visiwa vya bahari ya China Kusini, ingawa amesema kuwa Ufilipino na Marekani kamwe hazitoweza kuibuka washindi katika vita vyao dhidi ya China.

Akiashiria mkataba wa kiulinzi wa serikali ya Manila na Washington amesema: “Mara zote Wamarekani wamekuwa wakituwekea mashinikizo juu ya China na kutuinamisha vichwa, wanadhania kwamba Wafilipino ni  wadudu wa ardhini.” Akiendelea kufafanua suala hilo, Rais Duterte ameitaka Marekani kuwa ya kwanza kuingia vitani na China kwa kusema: “Leteni ndege na meli zenu bahari ya China Kusini. Anzeni kufyatua risasi na kisha sisi tuta kuwa wa pili baada yenu.” Rais wa Ufilipino ametoa natija kwa kusema kuwa, vita na makabiliano na China havina faida na kwamba Washington na Manila kamwe haziwezi kuibuka washindi katika vita hivyo mbele ya China. Pamoja na mambo mengine matamshi ya Rais Rodrigo Duterte wa Ufilipino ni uthibitisho tosha juu ya uungani mkono wa siasa za kupenda vita za Marekani katika bahari ya China Kusini. Aidha kukiri rais huyo wa Ufilipino juu ya mashinikizo ya Marekani dhidi ya nchi yake, kunabainisha uwepo wa mipango ya uchochezi wa Marekani kwa nchi zenye kugombania maeneo ya bahari ya China Kusini ili kuzisukuma nchi hizo ziingie vitani na nchi ya China.

Hata hivyo licha ya kwamba nchi nyingi za eneo kama vile Ufilipino, Vietnam, Malaysia na Brunei zimekuwa na mzozo na China kuhusiana na umiliki wa visiwa vya bahari ya China Kusini, lakini hakuna nchi mojawapo ambayo hadi sasa imewahi kutoa matamshi ya kutaka utatuzi wa kadhia hiyo kwa njia ya kijeshi kinyume na njia ya udiplomasia. Mashinikizo ya Marekani kwa serikali ya Ufilipino yaliifanya nchi hiyo ya Asia kuishtaki China katika Mahkama ya Kimataifa ya The Hague mwaka 2013 kuhusiana na uhalali wa umiliki wa visiwa vya bahari ya China Kusini. Kufuatia suala hilo mwaka 2016, mahkama hiyo ilitoa hukumu ambayo iliikabidhi serikali ya Manila uhalali wa udhibiti wa visiwa hivyo. Hata hivyo na licha ya hukumu hiyo, serikali ya Ufilipino si tu kwamba haijachukua hatua yoyote ya kukabiliana na Beijing, bali imezidi kuimarisha uhusiano wake na China kuliko wakati wowote ule. Mienendo hiyo ya Ufilipino inaonyesha kwamba, kinyume na harakati za Marekani, serikali ya Manila imefahamu vyema kwamba nafasi na uwezo wake haviiruhusu nchi hiyo kuweza kuingia katika mvutano wa kijeshi na China yenye idadi kubwa ya watu na nchi ya pili tajiri zaidi duniani. Ni kwa ajili hiyo tunaweza kusema kuwa misimamo ya Rais Rodrigo Duterte wa Ufilipino inaonyesha wazi kwamba uungaji mkono wa Washington kwa Ufilipino na nchi nyingine zenye mzozo na China, hauna lengo la kuzitetea nchi hizo mbele ya Beijing, bali una maana ya kufuatilia maslahi yake binafsi.

Ni kwa ajili hiyo ndio maana weledi wa mambo wanaamini kwamba nchi nyingi hazina nia ya kuingia kwenye mzozo na China kama ambavyo hazipo tayari kufuata siasa za kupenda mivutano za Marekani katika eneo. Katika uwanja huo, Hag Wayt, muhadhiri wa kitivo cha uchunguzi wa kiulinzi na kistratijia cha Australia anasema: “Miongoni mwa mambo yanayoonyesha kutofanikiwa stratijia za sasa za Marekani kuhusiana na China, ni misimamo ya nchi za Asia-Pasifiki. Katika eneo hili, marafiki na waungaji mkono wa Marekani hata kama wanahisi wasi wasi kutokana na uwezo mkubwa wa kila siku wa Beijing, lakini katika uhalisia wa mambo wanakabiliwa na changamoto iwapo watakata uhusiano wao na China. Na ndio maana nchi hizo zipo tayari kuendeleza urafiki wao na Beijing.” Hata hivyo ukweli ni kwamba sababu ya nchi zenye mzozo na China kutoiamini Marekani, ni misimamo yenye kugongana ya Washington. Hii ni kusema kuwa Ufilipino ni moja ya nchi za kusini mashariki mwa Asia ambayo kama zilivyo makumi ya nchi nyingi waitifaki wa Marekani hazikuambulia faida yoyote kutoka kwa Marekani ghairi ya umasikini. Aidha sababu nyingine iliyozifanya nchi hizo kuendelea kushirikiana na China ni siasa chanya na ushirikiano wa Beijing na nchi hizo. Katika miaka ya hivi karibuni China imewekeza kwa kiwango kikubwa katika nchi hizo kama vile Malaysia, Ufilipino, Vietnam, Indonesia, Cambodia na kadhalika, suala ambalo limezivutia nchi hizo kuweza kuendelea mahusiano yao mema na Beijing.

CHANZO: PARS TODAY

error: Content is protected !!