Ongezeko la ukatili nchini Mexico kwa silaha na vyanzo vya kifedha vya Marekani

Ongezeko la ukatili nchini Mexico kwa silaha na vyanzo vya kifedha vya Marekani

Kufuatia kushadidi machafuko na vitendo vya ukatili nchini Mexico, Rais Enrique Peña Nieto wa nchi hiyo amesema kuwa, kuwepo makundi ya jinai yanayotumia silaha na vyanzo vya kifedha vya Marekani, ndicho chanzo cha kuenea vitendo hivyo nchini humo.

Rais Peña Nieto ameashiria kwamba makundi ya uhalifu na yanayofanya magendo nchini Mexico kwa kutumia silaha na vyanzo vya kifedha, chimbuko lake ni Marekani na hivyo amesisitizia ulazima wa kuwepo ushirikiano kati ya nchi hiyo na Marekani katika kupambana na hali hiyo. Matamshi ya Rais Enrique Peña Nieto wa Mexico yametolewa katika hali ambayo kwa mujibu wa takwimu rasmi, vitendo vya mauaji nchini humo vimeongezeka katika nusu ya mwanzo ya mwaka huu kufikia asilimia 16 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita wa 2017. Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Mexico, katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, karibu kesi elfu 16 za mauaji zilisajiliwa kiwango ambacho ni cha juu zaidi,  kwa kuzingatia ripoti zinazohusiana na mauaji  hayo kuanzia mwaka 1997.

Mauaji ya kigaidi yameongezeka nchini Mexico

Hata kama ongezeko la vitendo vya ukatili limeshika kasi kutokana na kupanuka kwa harakati za magenge yanayoendesha magendo ya madawa ya kulevya na silaha nchini humo, lakini sababu nyingine kama vile kupakana na Marekani na kadhalika siasa za nchi hiyo, ni miongoni mwa sababu muhimu zinazotajwa katika uwanja huo, kadiri kwamba ongezeko la matumizi ya silaha za moto na madawa ya kulevya nchini Marekani na kutoshirikiana Washington na serikali ya Mexico City katika kupambana na magenge yanayofanya ulanguzi wa madawa ya kulevya, kumeongeza kwa kiwango kikubwa shughuli za magenge hayo. Hali hiyo imeongezeka hususan katika miaka ya hivi karibuni na baada ya kufanywa kuwa huru suala la ununuzi wa silaha nchini Marekani kuanzia mwaka 2005. Kuhusiana na suala hilo, Luis Videgaray, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mexico anasema: “Nchi mbili za Marekani na Mexico ni lazima zitumie ushirikiano wao kuhitimisha mwenendo wa magendo ya madawa ya kulevya na silaha kati yao.” Suala hilo linajiri katika hali ambayo katika miezi ya hivi karibuni, misimamo na siasa za Rais Donald Trump wa Marekani za kudhibiti zaidi mipaka ya Marekani na sisitizo lake la kujengwa ukuta kwa wa kuwazuia wahajiri kuingia nchini humo, limeharibu uhusiano wa nchi mbili.

Kupakana Mecico na Marekani, ni sababu ya ongezeko la machafuko nchini Mexico

Katika upande wa pili hali ya usalama wa Mexico pia inaathiriwa moja kwa moja na matukio ya ndani. Kuharibika hali ya kiuchumi ya nchi hiyo na pia kuongezeka kiwango cha ufisadi, ni sababu inayowasukuma raia wengi wa nchi hiyo kujiunga na makundi ya wafanya magendo ya madawa ya kulevya na silaha. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, zaidi ya watu milioni 53 nchini Mexico ni masikini. Suala hilo limepelekea weledi wengi wa masuala ya kisiasa kutaja ongezeko la vitendo vya jinai nchini humo kuwa ni matokeo ya utendaji mbovu wa serikali katika uga wa kiuchumi na kudhoofika uwezo wa jeshi la polisi katika kupambana na mitandao yenye nguvu inayojishughulisha na magendo ya madawa ya kulevya na silaha. Aidha kuendelea wimbi la utumiaji mabavu nchini humo, ni tishio kubwa kwa usalama wa raia wa Mexico. Kwa kutilia maanani hali hiyo, viongozi wa nchi hiyo wanapasa kuchukua hatua za lazima ndani na nje ya mipaka yao kwa ajili ya kupambana na magenge yanayoendesha magendo ya madawa ya kulevya na silaha. Katika uwanja huo, Andrés Manuel López Obrador, Rais Mteule wa Mexico ameahidi kutatua matatizo ya kijamii na kiuchumi ili kuiokoa nchi hiyo kutokana na tatizo la madawa ya kulevya.

error: Content is protected !!