Muungano wa wafanyakazi Tunisia waitisha mgomo wa nchi nzima

Muungano wenye nguvu wa wafanyakazi nchini Tunisia UGTT jana (Jumamosi) ulitoa mwito wa kufanyika mgomo wa nchi nzima wa siku mbili mwezi ujao wa Februari ili kushinikiza kupandishwa mishahara ya wafanyakazi laki sita na sabiini elfu (670,000) wa sekta ya umma.

Huduma za reli, mabasi, anga na nyinginezo zote zilisimama nchini Tunisia siku ya Alkhamisi huku mitaa ikijaa waandamanaji katika mgomo wa nchi nzima ulioitishwa kuishinikiza serikali iliyokataa kuwapandishia mishahara wafanyakazi wa umma.

Mkuu wa muungano huo wa vyama vya wafanyakazi, Nourredine Taboubi amewaambia waandishi wa habari kuwa, “baada ya kushindwa mazungumzo na serikali…, UGTT imeamua kuitisha mgomo mwingine wa nchi nzima tarehe 20 na 21 mwezi ujao wa Februari.”

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, uamuzi huo utaongeza mashinikizo kwa serikali ambayo hivi sasa inafanya juhudi za kufufua uchumi wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika ulioharibika vibaya.

Kwa mujibu wa Reuters, serikali ya Tunisia iko chini mashinikizo pia ya IMF inayoitaka isimamishe kutoa mishahara ya sekta ya umma, kama njia ya kupunguza nakisi ya bajeti yake.

Serikali ya Tunisia inasema haina fedha za kuweza kuwaongezea mishahara wafanyakazi wanaogoma ambao wanataka nyongeza ya dola milioni 850 za Kimarekani.

Mgogoro wa kiuchumi umevuruga viwango vya maisha nchini Tunisia. Kiwango cha watu wasio na kazi ni kikubwa kama ambavyo mkwamo wa kisiasa nao umezuia marekebisho ya kuvutia wawekezaji na kuandaa nafasi mpya za kazi. Serikali ya Tunisia imechukua hatua za marekebisho ya kiuchumi ili kuwafurahisha wafadhili na wakopeshaji kama vile IMF, tab’an inaonekana marekebisho hayo ni kwa madhara ya mwananchi wa kawaida.

error: Content is protected !!