Moto wa sigara umekatisha uhai wa mtu mmoja mwenye umri wa miaka 49

MOTO wa sigara umekatisha uhai wa mtu mmoja mwenye umri wa miaka 49, aliyetambulika kwa jina la Mwadini Mussa Yussuf mkaazi wa Mkele Unguja.

Hayo yalithibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa mjini magharibi Unguja, Thobias Sedoyeka, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Madema.

Alisema nyumba aliyokuwa akiishi marehemu huyo iliungua moto sehemu ya chumba chake na kusababisha kifo chake.

“Chanzo cha moto huo inasadikiwa kuwa ni sigara alizokuwa akivuta wakati akiwa amelewa na kuunguza godoro alilokuwa amelalia,” alisema.

Sambamba na hayo alisema, kwa wiki iliyopita makosa sita ya udhalilishaji yaliripotiwa katika mkoa huo.

Alifahamisha kuwa, kati ya makosa hayo kubaka ni makosa mawili, kulawiti mawili, kuingiliwa kinyume na maumbile kosa moja na kutorosha moja.

Aidha alifahamisha kuwa, kufuatia makosa hayo ya udhalilishaji, watuhumiwa wawili wamekamatwa na kufikishwa katika vituo vya polisi Madema na Mawanakwerekwe kwa hatua za kisheria.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!