Mogherini: EU kuzindua mfumo wa mabadilishano ya fedha baina ya Iran na Ulaya karibuni

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema mfumo maalumu kwa ajili ya mabadilishano ya fedha kati ya Iran na Ulaya kwa kifupi SPV utazinduliwa ndani ya siku chache zijazo.

Federica Mogherini ameyasema hayo katika kikao na waandishi wa habari mjini Brussels Ubelgiji jana Jumatatu na kufafanua kuwa, “Natumai mfumo huu utazinduliwa ndani ya wiki chache zijazo kabla ya kumalizika mwaka, ili kuimarisha na kulinda biashara halali.”

Mbali na kusisitizia umuhimu wa kuanza kutekelezwa mfumo huo, lakini pia kwa mara nyingine tena ameendelea kuunga mkono kikamilifu mapatano ya nyuklia yaliyofikiwa baina ya Iran na kundi la 5+1 yanayojulikana kwa kifupi kama JCPOA.

Kauli hiyo ya Mogherini imetolewa siku chache baada ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi kusema, “Kutokana na sababu maalumu, utaratibu wa utekelezaji mpango huo haujakamilika; lakini Tehran inatilia mkazo udharura wa pande zingine katika mpango huo kuchukua hatua zaidi kwa irada na uzito kamili ili mfumo wa mabadilishano ya fedha kati ya pande mbili uanze kutekelezwa.”

Itakumbukwa kuwa Jumanne ya tarehe 8 Mei mwaka huu, rais wa Marekani, Donald Trump aliitoa nchi yake katika mapatano hayo ukiwa ni uvunjaji wa wazi kabisa wa makubaliano ya kimataifa hasa kwa kuzingatia kuwa mapatano ya JCPOA yana baraka kamili za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na yalichukua miaka mingi kufikiwa. 

Baada ya kuitoa nchi yake kwenye mapatano hayo, Trump alitangaza kuirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyoondolewa baada ya kufikiwa mapatano hayo, na mpango huu wa SPV unakusudia kukwepa mtego wa vikwazo hivyo.

error: Content is protected !!