Mfumko wa bei washuka

KASI ya mfumko wa bei kwa mwaka ulioishia Januari 2019, imeshuka hadi asilimia ya 3.0 ukilinganisha na asilimia 3.5 kwa mwezi Disemba 2018.

Hayo yalielezwa na Mkuu wa Kitengo cha Takwimu za Bei Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Khamis Abdulrahaman Msham, wakati akizungumza na waandishi wa habari jana.

Alisema, mfumko wa bei za vyakula na vinywaji visivyo na vilevi uliongezeka na kufikia 3.6 mwezi Januari kutoka 2.2 mwezi Disemba 2018.

Alisema, faharisi za jumla za bei ziliongezeka hadi 108.3 mwezi Januari 2019 kulinganishwa na 105.2 mwezi wa Januari 2018.

Alisema, mfumko wa bei wa mwaka wa vyakula uliongezeka hadi asilimia 3.7 kwa mwaka ulioishia Januari 2019, ikilinganishwa na asilimia 2.3 mwezi Disemba 2018.

Alisema, faharisi za bei za vyakula ziliongezeka na kufikia 105.5 mwezi Januari 2019 ikilinganishwa na 101.7 mwezi Januari 2018.

Aidha, alisema mfumko wa bei wa mwaka kwa bidhaa zisizokuwa za vyakula uliteremka hadi 2.4 mwezi Januari 2019, ikilinganishwa na 4.3 mwezi Disemba 2018.

Alizitaja bidhaa zilizochangia kushuka kwa mfumko wa bei wa mwaka zilikuwa ni mchele wa Mbeya (7.8%), unga wa ngano (17.6%), samaki (2.7%), ndizi za mkono mmoja (11.7%) na sukari (4.4%).

Kwa upande wa mfumko wa bei wa mwezi Januari 2019, ulishuka kwa asilimia 0.4 ukilinganisha na asilimia 0.6 mwezi Disemba.

Alisema, mfumko wa bei wa vyakula na vinywaji visivyokuwa na vilevi kwa Januari 2019, ulishuka kwa asilimia 1.1 ukilinganisha na 1.6 mwezi Disemba 2018.

Alisema kushuka kwa mfumko wa bei wa mwezi kulichangiwa na bidhaa  kama mchele wa mapembe (0.7%), samaki (8.7%), mafuta ya taa (8.2%), petroli (5.7%), na diseli (8.1).

Mkuu wa Takwimu za Kiuchumi Ofisi ya Mtakwimu Mkuu, Abdulrauf Ramadhan Abeid, alisema, bado mfumko unaendelea kubakia chini ya tarakimu moja katika nchi za Afrika Mashariki na hivyo kwenda vizuri kiuchumi.

error: Content is protected !!