Mfumko wa bei washuka

KASI ya mfumko wa bei kwa mwaka uliomalizikia Juni 2019, imeshuka kufikia asilimia 2.7 ikilinganishwa na asilimia 3.1 mwezi uliomalizikia  Mei 2019.

Mfumko wa bei za vyakula na vinywaji visivyokuwa na vilevi uliongezeka kufikia asilimia 2.4 mwezi Juni 2019 kutoka asilimia 2.3 mwezi Mei.

Akizungumza na waandishi wa habari Mazizini, Mkuu wa Kitengo cha Takwimu za Bei, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Khamis Abdulrahman Msham, alisema, faharisi za bei kwa ujumla ziliongezeka hadi 111.31 mwezi Juni 2019, ikilinganishwa na 108.4 mwezi Juni 2018.

Alisema, kiwango cha mfumko wa bei za vyakula kiliongezeka hadi asilimia 2.4 kwa mwaka uliomalizikia Juni, ikilinganishwa na asilimia 2.3 mwezi Mei 2019.

Alisema, faharisi za bei za vyakula ziliongezeka kufikia 110.5 mwezi Juni ikilinganishwa na 107.9 mwezi Juni 2018.

Kasi ya mfumko wa bei wa mwaka kwa bidhaa zisizokuwa za vyakula ilishuka hadi 2.9 mwezi Juni 2019 ikilinganishwa na 3.6 mwezi Mei 2019.

Alisema faharisi za bei kwa bidhaa  zisizokuwa za vyakula ilifikia 111.9 mwezi Juni 2019 ikilinganishwa na 108 mwezi Juni 2018.

Alizitaja bidhaa zilizochangia kushuka kwa kiwango cha mwaka cha mfumko zilikuwa ni pamoja na mchele wa Mbeya (6.8%), samaki (7.3%), ndizi za mtwike (17.6%), ndizi za mkono mmoja (17.7%), na mafuta ya taa (0,6).

Kwa upande wa mfumko wa mwezi, ulishuka hadi 0.4 mwezi Juni 2019 ukilinganisha na 1.7 mwezi uliomalizikia Mei 2019.

Mfumko wa bei wa vyakula na vinywaji visivyo na vilevi kwa mwaka uliomalizikia Juni 2019, ulifikia asilimia 1.0 ikilinganishwa na 2.8 mwezi Mei 2019.

Kushuka kwa mfumko wa bei wa mwezi ulichangiwa na bidhaa kama mchele wa mapembe (3.2%), mchele wa basmati (0.3%), samaki (5.0%), ndizi za mtwike (6.3%), ndizi za mkono mmoja (8.5%), na saruji (2.9%).

Mkuu wa Takwimu za Kiuchumi, Abdulrauf Ramadhan Abeid, alisema, kasi ya mfumko kwa mwezi Juni 2019 kwa nchi za Kenya na Uganda, imepanda kidogo ikilinganishwa na Mei.

Alisema nchi ya Kenya mfumko ulifikia  asilimia 5.70 ikilinganishwa na 5.49 wakati Uganda ulikuwa asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.3.

Hata hivyo, alisema, kiujumla kasi ya mfumko kwa ukanda wa Afrika Mashariki bado ipo vizuri kutokana na kuendelea kubakia kwenye tarakimu moja.

Naye Mhadhiri wa Uchumi kutoka Skuli ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Chwaka, Dk.Suleiman Simai Msaraka,alisema, hali ya uchumi inaendelea vizuri na kinachohitajika ni kuwepo kwa uzalishaji wa bidhaa zaidi.

Meneja Msaidizi Idara ya Uchumi Benki Kuu tawi la Zanzibar, Moto Ng’winganele Lugobi, alisema, pamoja na kasi ya mfumko huo kuongezeka, bado Zanzibar imefikia hatua nzuri kulinganisha na malengo yaliyowekwa ya kuwepo kwa tarakimu moja ya mfumko wa bei kwa nchi za Afrika Mashariki.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!