Meli Mpya ‘Sea Star1’ yenye uwezo wa kubeba abiria 1500 yawasili Zanzibar

Meli Mpya ya Kampuni ya Usafiri wa Baharini ya Sea Star  yenye uwezo wa kubeba Mizigo Tani 1,400 na Abiria 1,500  imewasili Bandarini Zanzibar kwa ajili ya kuongeza huduma za Usafiri wa Baharini katika Mwambao wa Bahari ya Afrika Mashariki.

Meli hiyo iliyopewa jina la Sea Star 1 itafuatiwa na Boti nyengine Mbili za Mwendo  Kasi zinazotarajiwa kuingia Visiwani Zanzibar Mwezi Juni Mwaka ujao wa 2019.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa na baadhi ya Viongozi na Watendaji wa Mamlaka zinazosimmamia Usafiri wa Baharini alipata nafasi ya kukagua sehemu mbali mbali za Meli hiyo iliyopo Bandarini Malindi na kuridhika na Ubora wake.

Meli hiyo yenye sehemu kubwa yakubebea Mizigo, Vyumba vya Watu Mashuhuri { VIP} pamoja na Abiria wa kawaidaitaanza  safari za Unguja-Pemba – Tanga, Zanzibar – Dar es salaa, Zanzibar– Mtwara na baadae kuendelea na safari za mbali kwa kuanzia Visiwa vya Comoro.

Sehemu kubwa ya kuwekea Mizigo mbali mbali ndani ya Meli Mpya ya Sea Star yenye uwezo wa kubeba mizigo Tani 1,400 na Abiria 1,500 ikiwepo Bandarini Malindi.

Safari ya Zanzibar – Dar es salaam huchukuwa muda unaokadiriwa wastan wa saa Tatu wakati safari ya Unguja – Pemba itachukuwa wastani wa saa Nne na Nusu.

Akitoa Maelezo ya uwepo wa Meli hiyo Nchini Mwakilishi wa Kampuni ya Sea Star Mh. Salum Turky alisema Uongozi wa Kampuni hiyo umejizatiti kutoa huduma bora za Usafiri wa Baharini kwa Wananchi wote.

Mh. Turky amesema miongoni mwa mambo yatakayozingatiwa na Uongozi huo katika uendeshaji wa Biashara hiyo ni kuhusika katika  kufuata taratibu zote zilizoainishwa na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini.

Amesema Abiria wa kawaida atawajibika kulipia nauli shilingi 25,000/, Mtoto wa kawaida atalipiwa Nusu Nauli na yule aliye na umri kati ya siku Moja hadi Miaka Sita atachukuliwa bila ya malipo.

Mh. Salum Turky amemueleza Balozi Seif  kwamba Uongozi huo umeahidi kuunganisha safari za Visiwa vya Comoro kufuatia ahadi aliyoitoa  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein katika kuimarisha uhusiano kati ya Zanzibar na Visiwa hivyo.

Katika kuimarisha huduma hizo za Usafiri wa Baharini Mwakilishi huyo wa Sea Star aliiomba Serikali kuwapatia sehemu Maalum na ya uhakika kwa ajili ya kuuzia Tiketi ili kuwaondoshea usumbufu Wananchi wanaohitaji huduma hizo.

Naye  Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda Zanzibar Mh. Hassan Khamis Hafidh aliushauri Uongozi wa Sea Star kwenda na  ushindani wa Kibiashara huku pia wakizingatia huduma nafuu kwa Wananchi.

Mh. Hassan amesema Serikali imeamua kuweka milango wazi ya uwekezaji Nchini katika azma ya kuona maeneo yote ya huduma za Umma yanawafikia vyema na kwa wakati Wananchi walio wengi hasa wale wenye kipato cha chini.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Kampuni hiyo ya Kizalendo kwa uwamuzi wake wa kuongeza huduma za Usafiri wa Baharini Nchini.

Balozi Seif  amesema uamuzi wa Kampuni hiyo wa kuimarisha huduma za Usafiri umekuja kwa wakati huku ukizingatia kwenda sambamba na mabadiliko ya maisha ya Wananchi yanayowapa fursa ya kuingia katika mzunguuko wa kibiashara unaohitaji zaidi huduma za usafiri.

Kampuni ya Sea Star iliwahi kumiliki Boti Mbili ziendazo kwa kasi za Sea Star One na Sea Star Two zilizotoa hudumaza usafiri wa Baharini kati ya Bandari ya Zanzibar na ile ya Dar es salaam kwazaidi ya Miaka 13.

error: Content is protected !!