Mauaji Sudan yanaendelea, 11 wauawa 20 wajeruhiwa Darfur

Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan imetangaza habari ya kuuawa watu 11 na kujeruhiwa wengine 20 katika machafuko yaliyotokea kwenye eneo la al Dalij la jimbo la Darfur, magharibi mwa nchi hiyo.

Vyombo vya habari vya Sudan vimeinukuu kamati hiyo ikisema katika taarifa yake kwamba, watu 9 kati ya raia hao wa Sudan wameuliwa na wanamgambo wenye mfungamano na jeshi la nchi hiyo kwa kupigwa risasi na marungu. Sababu za vifo za watu wengine wawili kati ya hao 11 haikutangazwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan imesema kuwa wanamgambo wa jeshi la nchi hiyo ndio waliofanya mashambulizi hayo katika kijiji cha al Dalij cha katikati mwa Darfur na kusisitiza kuwa, wanamgambo hao wamewashambulia raia hao kwa amri ya jeshi la Sudan.

Baadhi ya wakazi wa Darfur

Tarehe 11 Aprili mwaka huu, jeshi la Sudan lilitangaza kumpindua Jenerali Omar al Bashir baada ya kutozuilika tena maandamano makubwa ya nchi nzima ya wananchi wa nchi hiyo waliokuwa wamachoshwa na ukandamizaji wa serikali ya Omar al Bashir iliyodumu kwa takriban miaka 30. 

Licha ya jeshi la Sudan kufanya mapinduzi hayo ya kijeshi, lakini wananchi wa Sudan hadi hivi sasa wanaendelea na maandamano yao wakilitaka jeshi likabidhi madaraka kwa raia.

Mnamo Juni 3 wanajeshi wa Sudan waliwapiga risasi na kuwaua raia zaidi ya 100 ambao walikuwa wamekusanyika na kufanya mgomo wa kukaa chini nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum wakitaka baraza la kijeshi liondoke madarakani.

error: Content is protected !!