Mama, mtoto wafariki baada ya kugongwa na gari

MAMA na mtoto wake wamefariki katika hospitali ya Mnazimmoja wakati wakipatiwa matibabu, baada ya  kugongwa na gari katika barabara ya Melinne njia ya Uzi, wakati wakivuka barabara.

Tukio hilo lilitokea Januari 16 saa 11:30 asubuhi wakati gari yenye namba Z 307 JU, ambayo ilikuwa ikiendeshwa na Mteza Ali Hamdu (42) ambae alikuwa anatokea Mwanakwerekwe kuelekea Fuoni, kuwagonga.

Akizungumza kwa njia ya simu, Mkaguzi msaidizi wa polisi, Mohammed Talhata Fumu, aliwataka madereva kuwa makini wanapokuwa barabarani ili kudhibiti ajali.

Alisema gari hiyo ilikua inaenda chukua wafanya kazi wa hotelini na kufika maeneo hayo iliwagonga watembea kwa miguu na kusababisha vifo vyao.

Aiwataja marehemu  kuwa ni Khadija Abdi  Ramadhani (28) wa Melinne na mtoto  wake, Mahmoud Haji Hassan mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi minane.

“Nawasihi madereva na wananchi kwa ujumla kuwa waangalifu wanapotumia barabara ili kuepusha ajali,” alisema.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!