Mahakama Nigeria yakataa kumuachia huru kwa dhamana Sheikh Zakzaky

Mahakama nchini Nigeria imekataa kumwachia huru kwa dhamana kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchini humo Sheikh Ibrahim Zakzaky siku kadhaa baada ya wafuasi wake zaidi ya 40 kuuawa katika maandamano waliyofanya kutaka kuachiwa huru kiongozi huyo wa kidini.

Sheikh Zakzaky ambaye ni kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) amekuwa kizuizini tangu mwezi Disemba mwaka 2015 na mwezi Aprili alishtakiwa kwa tuhuma za mauaji, kuitisha mkusanyiko kinyume cha sheria, kuvuruga amani ya nchi na nyinginezo. Sheikh Zakzaky amekanusha tuhuma zote hizo.

Maxwell Kyon wakili anayemtetea kiongozi huyo wa kidini amesema kuwa mahakama imekataa kumwachia huru kwa dhamana mteja wake.

Timu ya kisheria inayomtetea Sheikh Zakzaky imetaka kuachiwa huru mwanazuoni huyo ikisema kuwa anasumbuliwa na matatizo ya kiafya ambayo yanahitaji matibabu nje ya nchi. Hata hivyo mahakama imepinga ombi hilo.

Mahakama Kuu ya jimbo la Kaduna kaskazini mwa Nigeria jana ilidai kuwa hakuna ushahidi wa maana uliowasilishwa mahakamani ili kuweza kumwachia kwa dhamana Sheikh Ibrahim Zakzaky.

error: Content is protected !!