Mafuriko yaua watu 66 nchini Msumbiji

Watu wasiopunfua 66 wamepoteza maisha na laki moja na 41 elfu wameathirika kutokana na mvua kubwa zilizoyakumba maeneo ya katikati na kaskazini mwa Msumbiji. Serikali ya Msumbiji imetoa takwimu hizo na kuomba misaada ya kimataifa kukabiliana na janga hilo la kimaumbile.

Msemaji wa serikali ya Msumbiji, Bi Ana Comoana amesema kuwa Maputo imetangaza hali ya hatari kutokana na kwamba mvua zinaendelea kunyesha huku utabiri ukionesha kuwa kimbunga cha Idai kitaikumba nchi hiyo ya kusini mwa Afrika baina ya kesho Alkhamisi au keshokutwa Ijumaa.

Alisema hayo mbele ya waandishi wa habari baada ya Baraza la Mawaziri la Msumbiji kukutana mjini Maputo kwa ajili ya kujadili mafuriko hayo makubwa sana.

Msemaji wa serikali ya Msumbiji, Bi Ana Comoana

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa serikali ya Msumbiji, mafuriko katika nchi hiyo maskini zaidi barani Afrika yameshaharibu nyumba 5,756 na kuathiri mali nyingi huku watu 141,325 wakiathiriwa moja kwa moja na maafa hayo. Zaidi ya watu 111 wamejeruhiwa, hospitali 18 zimeharibiwa, madarasa 938 ya shule nayo yameharibiwa kikamilifu wanafunzi 9763 wakiathiriwa na mafuriko hayo. Zaidi ya mashamba 168,000 ya mazao yameharibiwa kabisa kwa mujibu wa msemaji huyo wa serikali ya Msumbiji ambaye amesema kuwa. serikali imetoa amri kwa watu wanaoishi mabondeni wahame maeneo hayo ili kuokoa maisha yao.

Kabla ya hapo, Ofisi ya Uratibu ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilikuwa imeripoti kwamba, watu sita wameaga dunia baada ya kusombwa na mafuriko katika mkoa wa Tete wa katikati mwa Msumbiji. Aidha watu wengine wanne wamefariki dunia kutokana na janga hilo la kimaumbile katika mkoa wa pwani wa Zambezia.

error: Content is protected !!