Leseni za walimu wasio na sifa kusitishwa

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali, inakusudia kusitisha utoaji wa leseni kwa walimu ambao hawajasomea fani hiyo, pale tu sheria mpya itakapopitishwa.

Kaimu Mrajisi wa elimu Zanzibar, Thneyuu Mabrouk Hassan, alisema hayo wakati akizungumza na gazeti la Zanzibar leo, ofisini kwake Vuga.

Alisema, wakati umefika wa kuifunga milango ya walimu ambao hawajasomea ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora.

Aidha, alisema wanaendelea na utaratibu wa kutoa leseni kwa walimu wote kwa muda wa mwaka mmoja hadi pale sheria hiyo mpya itakapopitishwa.

“Tulikuwa tukitoa leseni kwa muda wa miaka mitatu kwa walimu wote lakini hivi sasa tunawapa kwa muda wa mwaka mmoja tu, na pale sheria itakapopitishwa basi tutaanza kuzuia ili waweze kujirekebisha na kusomea ualimu,”alisema.

Alisema hadi sasa ofisi yao imetoa leseni 9,700 kwa walimu wa skuli za serikali na binafsi.

Alisema walimu wote ambao hawajasomea fani hiyo watapewa muda wa mwaka mmoja ili kusoma ili watambulike kisheria.

Aliwasisitiza walimu hao kusoma katika vyuo vinavyotambulika na wizara ambavyo vimesajiliwa kisheria ili kuepusha kukosa leseni.

Alivitaja vyuo ambavyo vimesajiliwa na vinavyotambulika kisheria na wizara, ni pamoja na Zanzibar College, Aghakan Foundation, Al-Sumait na Madrasa Resource Center.

“Hatutakuwa tayari kumpa mtu leseni ambaye amesoma katika vyuo ambavyo havina sifa, vipo vyuo vingi vinavyoanzishwa ambavyo havina sifa na wazazi wanakubali watoto wao kujiunga na kupoteza pesa zao,” alisema.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!