Kustaafu Mkemia kwaathiri kesi dawa za kulevya

KUSTAAFU kwa mtaalamu wa uchunguzi wa dawa za kulevya Faridi, kumepelekea kupelekwa mbele kesi ya kupatikana na dawa za kulevya inayomkabili kijana Masoud Faki Machela (27) mkaazi wa Kitope Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Mkoa wa Kaskazini Unguja, baada ya upande wa mashitaka kuomba tarehe nyengine.

Hakimu wa Mahakama ya Mkoa Mfenesini Nassor Ali Salim, alitoa tarehe hiyo baada ya upande wa mashitaka kueleza kwamba, shahidi huyo ameshastaafu kazi na kuiomba Mahakama ifanyiwe upya uchunguzi dawa hizo na ndipo shahidi awasilishwe Mahakamani hapo kwa ushahidi.

Kesi hiyo imefunguliwa Juni 20 mwaka huu ikiongozwa na Hakimu Nassor Ali Salim chini ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Safia Serembe, ambapo alisomewa shitaka lake mbele ya hakimu huyo.

Alidaiwa Mshitakiwa huyo alipatikana na kikopo cha plastiki rangi nyeupe kikiwa na maandishi ya ‘laser Tec Cotton Buds’, ndani yake mkiwa na kete 57 zenye unga wa dawa za kulevya aina ya heroini, zenye uzito wa 0.878 gms, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Mshitakiwa alidaiwa kukamatwa na dawa hizo siku ya tarehe 9 May mwaka huu mnamo majira ya saa 6:00 mchana  huko katika kijiji cha Ktope Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Mloa wa Kaskazini Unguja.

Aidha mshitakiwa ameshitakiwa chini ya kifungu cha 15 (1) (a) cha sheria namba 9 mwaka 2009, kama ilivyorekebishwa na kifungu cha 11(a) cha sheria namba 12 ya mwaka 2011 sheria za Zanzibar.

Hivyo upande wa Mashitaka unafanya jitihada ya kutafuta mkemia mwengine kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi upya kielelezo cha kesi hiyo, ili Mahakama kuendelea na kesi hiyo.

Mshitakiwa Masoud Faki Machera anatarajiwa kupandishwa tena Mahakamani hapo Januari 10 mwakani kwa ajili ya kusikilizwa.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!