Kuongezeka mashinikizo ya kubuniwa serikali ya kiraia nchini Sudan

Baada ya kupita karibu siku 10 tokea kupinduliwa Rais Omar al-Bashir wa Sudan na jeshi la nchi hiyo, vyama vya kisiasa vya nchi hiyo pamoja na mashirikaya kimataifa na ya kieneo yanashinikiza kukabidhiwa madaraka kwa serikali ya kiraia haraka iwezekanavyo. Kuhusiana na suala hilo, Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limetoa muhula wa siku 15 kwa ajili ya kukabidhiwa madaraka kwa serikali ya kiraia.

Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni Kuu ya Umoja wa Afrika ametangaza utayarifu wa umoja huo kwa ajili ya kutatua kwa amani mgogoro wa Sudan na kuongeza kuwa kikao cha dharura kitafanyika hivi karibuni kwa ajili ya kuchunguza matukio ya nchi hiyo. Matukio ya Sudan yamechukua mkondo mpya kufuatia hatua ya wanajeshi kumpindua Rais Omar al-Bashir na kubuni Baraza la Kijeshi la Mpito kwa ajili ya kuendesha masuala ya nchi hiyo.

Baraza hilo la kijeshi la mpito limetangaza kwamba kwa sasa litasimamia utekelezaji wa masuala yote ya kiuchumi na kisiasa ya nchi hiyo hadi pale hatua za lazima zitakapochukuliwa kwa ajili ya kubuniwa serikali itakayochaguliwa na wananchi. Viongozi wanajeshi wa baraza hilo wanasema utekelezaji wa jambo hilo utahitajia muda usiopungua mwaka mmoja.

Kuhusu hilo Jalal Deen Sheikh mmoja wa wanachama wa baraza hilo amesema kwamba baraza hilo la kijeshi la mpito litahitaji muda usiozidi miaka miwili kwa ajili ya kuandaa taratibu za kukabidhiwa raia madaraka.

Hii ni katika hali ambayo vyama vya siasa na wapinzani wana wasiwasi mkubwa kuhusu kuendelea kutawala wanajeshi nchini humo. Wanataka kuondolewa madarakani kwa wanajeshi wote wakongwe na vilevile waungaji mkono wa serikali ya al-Bashir. Wataalamu wa mambo na Wasudan waliowengi wanaamini kwamba hakuna dhamana yoyote ya wanajeshi kukabidhi madaraka kwa wanajeshi, hali ambayo imezidi kufanya mambo kuwa magumu.

Husni Ubeidi, Mkuu wa Kituo cha Utafiti cha Ulimwengu wa Kiarabu na Meditaranea anasema kuhusu suala hilo kwamba ni vigumu sana kutasawari kukabidhiwa madaraka kwa njia ya amani nchini Sudan. Hakuna dhamana yoyote ya kukabidhiwa madaraka serikali ya kiraia. Katika hali ambayo serikali ya mpito imewataka raia wote kukomesha maandamano mitaani, vyama vingi vya Sudan vimetangaza kwamba havitaacha kufanya maandamano hadi pale madaraka yatakapokabidhiwa kidemokrasia. Ni kwa msingi huo ndipo wapinzani wakaendelea kusalia barabarani huku wakipiga nara za, ‘uhuru’, ‘amani’, ‘uadilifu’ na ‘mapinduzi ya wananchi’. Huku umoja wa Afrika ukiwa umetoa muhula wa siku 15 kukabidhiwa madaraka kwa wananchi, wapinzani wa Sudan wanataka kubuniwa kwa serikali ya kiraia, kukamatwa na kuhukumiwa washirika wote wa al-Bashir.

Katika hali hiyo safari za baadhi ya maafisa na viongozi wa taasisi za kieneo na wa baadhi ya nchi kwa ajili ya kuonana na mkuu wa Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan zimezidisha wasiwasi nchini humo, hasa ikitiliwa maanani kwamba siasa za Omar al-Bashir zilikuwa zimepelekea kuongezeka kwa uingilia wa nchi za kigeni nchini humo. Vyama vingi vya nchi hiyo vina wasiwasi kwamba Marekani na washirika wake wanataka kutumia vibaya hali ya nchi hiyo kwa ajili ya kudhamini maslahi yao kupitia misaada mbalimbali kwa wanajeshi. katika kuthibitisha hilo gazeti la Rai al-Yaum limeashiria matukio yanayoenda kwa kasi nchini Sudan na kuchukua hatamu za uongozi wa Baraza la Kijeshi la Mpito Abdulfattah al-Burhan, ambaye ni muungaji mkono mkubwa wa kutumwa askari wa Sudan huko Yemen, na kusema kuwa jambo hilo linaashiria wazi uingiliaji wa Marekani na Saudi Arabia nchini humo. Jambo linaloonekana wazi ni kuwa nafasi ya wanajeshi na raia wa kawaida wa Sudan katika mustakbali wa kisiasa wa nchi hiyo itaweza kubainika wazi katika miezi kadhaa ijayo.

error: Content is protected !!