Kongo DR yatuma ombi rasmi la kuwa mwanachama wa EAC

Bendera ya jumuiya (kushoto) pamoja na bendera za nchi 5 za kwanza za EAC 

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetuma ombi rasmi la kutaka kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC.

Rais Felix Tshisekedi wa nchi hiyo amemuandikia barua Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye ndiye mwenyekiti wa kiduru wa jumuiya hiyo ya kikanda kwa sasa, akimuomba alizingatie ombi lake kwa msingi kuwa nchi yake imeendelea kuwa na uhusiano mkubwa na unaostawi na nchi za jumuiya hiyo.

Kwa mujibu wa Owora Richard Otieno, Mkuu wa Idara ya Habari na Uhusiano Mwema wa Sekritarieti ya EAC mjini Arusha Tanzania, nchi inapoomba uanachama wa jumuiya, mwenyekiti huwaagiza mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama kuitaarifu rasmi Sekritarieti ya jumuiya kuhusiana na ombi hilo.

Baada ya hapo Sekritarieti itawalisha ombi hilo kwenye mkutano ujao wa Baraza la Mawaziri la EAC ambalo litaunda kamati ya kutathmini na kupiga msasa ombi hilo kabla ya kukubaliwa au kukataliwa. Baraza hilo litatumia Sura ya Tatu ya Mkataba wa EAC kutathmini ombi hilo la Kinshasa.

Itakumbukwa kuwa, Machi 2016, viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki waliidhinisha kwa kauli moja Sudan Kusini kujiunga na jumuiya hiyo, katika mkutano wao uliofanyika mjini Arusha, Tanzania.

Kwa kuidhinishwa Sudan Kusini kuwa mwakachama wa 6 wa EAC, jumuiya hiyo ilifikisha idadi jumla ya watu milioni 162. Wanachama wengine wa EAC ni Rwanda, Kenya, Tanzania, Burundi na Uganda.

error: Content is protected !!