Jitihada za India za kupunguza utegemezi kwa dola ya Marekani

Wizara ya Biashara ya India imetangaza kuwa, nchi hiyo inafanya jitihada za kupunguza utegemezi wa nchi hiyo kwa sarafu ya dola ya Marekani.

Katika hatua za kupunguza matumizi ya sarafu ya dola katika biashara yake na nchi mbili washirika wakubwa wa India, Wizara ya Biashara ya nchi hiyo imeainisha bei kununua na kuuza sarafu ya Uturuki, lira na won ya Korea ya Kusini ili kurahisisha biashara kati yake na nchi hizo mbili. Taarifa ya wizara hiyo imesema, inatazamiwa kuwa hatua hiyo itapunguza gharama za kibenki na kurahisisha miamala ya kibiashara kati ya India na Korea ya Kusini na Uturuki. Awali India ilikuwa imetangaza kuwa inaazimia kutumia sarafu yake ya rupia katika biashara kati yake na China. Kwa kuzingatia kulegalega kwa hali ya dola katika masoko ya kimataifa si tu india bali nchi nyingine pia zimeanzisha mikakati ya kutumia fedha zao za kitaifa badala ya dola katika miamala yao ya kibiashara. Makubaliano yaliyofikiwa baina ya China na Japan, China na Russia na vilevile baina ya nchi wanachama wa kundi la Brics linaloundwa na Russia, India, China na Afrika Kusini kwa ajili ya kustafidi na sarafu za nchi hizo yanaweza kutathminiwa katika uwanja huo. Utumiaji wa sarafu za kitaifa si tu kuwa unarahisisha miamalama ya kibiashara kati ya nchi mbalimbali bali pia unazidisha uhuru na kujitegemea kiutendaji kwa taasisi za kifedha na kibiashara katika medani ya kimataifa. Khadija Karahan mchambuzi wa masuala ya kibiashara wa nchini Uturuki anasema: 

Nchi mbalimbali zimezidisha juhudi za kupunguza athari mbaya za kuyumbayumba kwa sarafu ya dola hususan baada ya mgogoro wa kifedha na kiuchumi ulioiathiri dunia mwaka 2008. Hivi sasa suala la kufikiwa lengo la kutumiwa sarafu za kitaifa katika biashara za nje limekuwa jambo lenye umuhimu mkubwa katika ukuaji wa kiuchumi. Kuhusiana na suala hilo, baadhi ya nchi za Ulaya na nchi kama Iran, Uturuki, Russia, China na India zinafanya jitihada za kutumia sarafu zao za kitaifa katika mfumo wa mabadilishano ya fedha wa kimataifa badala ya sarafu ya dola. 

Kwa kuzingatia kuweko hatarini nguvu ya Marekani duniani na kuongezeka mtikisiko wa dola katika masoko ya kimataifa nchi mbalimbali duniani zimefikia natija kuwa, zinaweza kufanya biashara kwa kutumia sarafu zao zenyewe na hivyo kupunguza utegemezi wao kwa dola ya Marekani. Japan ambayo ni muitifaki wa kistratejia wa Marekani mashariki mwa Asia na miongoni mwa nchi zenye uchumi ulionawiri duniani tayari imeanza kutumia sarafu yake ya yen katika miamala yake ya kibiashara. Hatua hiyo imetokana na Japan kutambua hatari ya kuanguka thamani ya dola.

Kuongezeka madeni ya Marekani ni miongoni mwa sababu za kujitokeza hali hiyo. Kiwango cha madeni ya serikali ya Marekani kimeongezeka sana katika miaka ya  karibuni, na sasa madeni hayo yamefikia dola trilioni 20, suala linaloifanya Marekani kuwa nchi yenye kiwango kikubwa cha madeni duniani. Kiwango hicho cha deni la Marekani kinatajwa kuwa sawa na kiwango jumla cha uzalishaji wa ndani wa nchi hiyo kwa mwaka mmoja. Karibu theluthi moja ya kiwango cha fedha hizo inazodaiwa Marekani ni mali ya benki kuu za nchi kadhaa, huku China ikidai dola trilioni 1.2 na Japan trilioni 1. Ongezeko hilo la madeni ya serikali ya Marekani limezusha wasiwasi kwa aghalabu ya wachumi wa kimataifa. Hii ni kwa sababu kama serikali ya nchi hiyo itashindwa kulipa madeni yake, athari za suala hilo zitakuwa na madhara makubwa kwa uchumi wote wa dunia. 

Ila Patnaik profesa wa masuala ya uchumi wa India anasema: Hatua ya nchi zinazostawi ya kutumia sarafu zao wa kitaifa katika miamala ya kibiashara imekuwa na umuhimu mkubwa katika miaka kadhaa ya karibuni na kuwa fikra mathubuti. Hivi sasa India pamoja na nchi nyingine sita zinatumia sarafu zao katika miamala ya kibiashara.

Bi Ila Patnaik, profesa wa masuala ya uchumi wa India 

Wasiwasi wa kulegalega sarafu ya dola umezifanya China na Russia ziutake Mfuko wa Fedha wa Kiamtaifa (IMF) kuanzisha sarafu ya aina moja itakayotumiwa na nchi zote. Hata hivyo kwa kuzingatia hitilafu za kisiasa zilizopo inaonekana kuwa haitakuwa jambo rahisi kufikiwa mapatano ya kimataifa ya kuanzisha sarafu moja ya kimataifa katika siku za usoni. Ndio maana nchi mbalimbali duniani zinafanya kila ziwezalo kutumia sarafu zao za kitaifa katika miamala yao ya kibiashara na pande nyingine, hatua ambayo inaweza kuwa na taathira mbaya kwa sarafu moja au kadhaa za kimataifa na hivyo kusababisha mageuzi makubwa katika mfumo wa biashara ya kimataifa.

error: Content is protected !!