Iran: Marekani inatumia tuhuma bandia ili kupanua soko la silaha zake

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema lengo la Marekani kuibua tuhuma zisizo na msingi na kueneza chuki dhidi ya Iran ni kupanua soko la silaha zake katika eneo la Asia Magharibi.

Bahram Qassemi aliyasema hayo jana Alkhamisi hapa mjini Tehran, ikiwa ni radimali kwa madai ya urongo yaliyotolewa hivi karibuni na Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani dhidi ya Iran.

Amesema, “Maafisa wa Marekani wakiwa chini ya mashinikizo ya lobi za Kizayuni wamekuwa wakieneza propaganda chafu dhidi ya Iran, ili kuonesha kuwa kuna mgogoro katika eneo la Asia Magharibi, na kwa mantiki hiyo waweze kuimarisha uuzaji wa silaha zao katika eneo.”

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema matamshi ya hivi karibuni ya Mike Pompeo yamechochewa na ghadhabu za kuendelea kuimarika uhusiano wa Iran na Iraq.

Siku ya Jumatano katika mazungumzo na Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini Houston, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alikariri madai hewa na yasiyo na msingi dhidi ya Iran, na kusema kuwa Tehran inaendeleza harakati haribifu katika eneo la Asia Magharibi.

Alidai kuwa, “Iran inatumia uuzaji wa nishati yake ili kuimarisha ushawishi usio na maana katika eneo lote la Mashariki ya Kati, hususan Iraq.”

Hii ni katika hali ambayo, baada ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hassan Rouhani kukamilisha safari yake ya siku tatu nchini Iran juzi Jumatano, Tehran na Baghdad zilitoa taarifa ya pamoja zikisisitiza kupanuliwa zaidi uhusiano wa nchi hizi mbili katika nyanja zote.

error: Content is protected !!