‘Iran haitakubali mazungumzo ambayo msingi wake ni mabavu na vitisho’

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema: “Iran haitakubali kufanya mazungumzo ambayo msingi wake ni utumiaji mabavu na vitisho.”

Majid Takht-Ravanchi Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa aliyasema hayo Jumanne katika mahojiano na Televisheni ya CNN na kuongeza kuwa: “Hivi sasa wakati ambao Marekani inaishinikiza Iran ni vipi inataraji kuwa Tehran itakubali pendekezo la mazungumzo chini ya mashinikizo.”

Takht-Ravanchi ameashiria kuhusu ripoti za baadhi ya vyombo vya habari  kuwa Marekani inalenga kutuma askari 120,000 kukabiliana na Iran katika eneo la Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) na kusema: “Kwa mtazamo wa Iran, hatua kama hizo ni vita vya kisaikolojia na Iran kamwe haitaki kuibua mapigano kwani mapigano katika eneo si kwa maslahi ya yeyote.”

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa pia amejibu madai kuwa eti Iran inafuatilia silaha za nyuklia kwa kusema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaki kumiliki silaha za nyuklia kwani inazitazama silaha hizo kuwa kinyume cha itikadi za Kiislamu. Aidha amesema silaha za nyuklia hazina nafasi yoyote katika stratijia na sera za kujihami za Iran.

error: Content is protected !!