Indhari ya kuongezeka idadi ya wakimbizi wanaokufa maji katika Bahari ya Mediterania

Bahari ya Mediterania ingali inaendelea kuwa machinjio ya roho za maelfu ya wakimbizi wanaofanya safari za hatari kuelekea Ulaya kwa matumaini ya kuishi maisha bora.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limetangaza katika ripoti yake mpya kwamba, katika mwaka huu wa 2018, wahajiri zaidi ya elfu mbili wamezama baharini wakati walipokuwa wanavuka bahari ya Mediterania kuelekea barani Ulaya. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, zaidi ya nusu ya wahajiri waliozama walikuwa wanaelekea nchini Italia. Charlie Yaxley, msemaji wa UNHCR amesema: Kwa muda wa miaka kadhaa, bahari ya Mediterania imekuwa ndiyo njia ya majini yenye kusababisha maafa makubwa zaidi ya roho za watu duniani kwa wakimbizi na wahajiri; na kuendelea kwa hali hiyo inapasa liwe jambo lisilokubalika kwa watu wote. Hatua kali za kisiasa na kiusalama zinazochukuliwa na serikali za nchi za Ulaya za kuzuia wahajiri na watafutao hifadhi kuingia barani Ulaya zimepelekea kupungua idadi ya wahajiri wanaoingia barani humo. Lakini idadi ya wakimbizi na wahajiri wanaokufa maji katika bahari ya Mediterania bado haijapungua.

Hali hii inatokana pia na siasa za nchi za Ulaya zinazokinzana na misingi ya kiutu na sheria za kimataifa. Serikali za Ulaya na Marekani hazilipi umuhimu suala la ubinadamu katika sera zao za kuzuia wahajiri na wakimbizi kuingia katika ardhi za nchi zao. Serikali za Ulaya na hasa Italia, ambayo ni moja ya mafikio makuu ya wahajiri, imefika hadi inazuia hata shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotetea haki za binadamu, za kutoa misaada kwa wakimbizi wanaotangatanga kwenye maji ya bahari ya Mediterenia. Katika matukio kadhaa, meli za mashirika yasiyo ya kiserikali, zilizobeba umati wa wakimbizi waliookolewa, zinabaki katika bahari ya Mediterenia kwa muda wa wiki kadhaa zikingojea kupatiwa kibali cha kuingia kwenye ardhi ya moja ya nchi hizo za Ulaya zinazojinasibu kuwa ni watetezi wa haki za binadamu. Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi amesema, shirika hilo lina wasiwasi mkubwa kutokana na vizuizi vya kisheria na kilojistiki yanavyowekea mashirika yasiyo ya kiserikali, yanayosaidia operesheni za uokozi na utoaji misaada katika bahari ya Mediterania. Hata hivyo wasiwasi huo na indhari hizo zilizotolewa na UNHCR hadi sasa hazijawa na taathira yoyote kwa sera na sheria kali zinazotekelewa na serikali za Ulaya na Marekani za kuzuia wahajiri na wakimbizi wasiingie katika nchi zao. Na ili kujiepusha na lawama za taasisi na jumuiya za kimataifa, baadhi ya nchi za Magharibi kama Marekani, Hungary na Austria zimeamua kujitoa kwenye mkataba wa kimataifa wa kulinda haki za wakimbizi.

Wahajiri kutoka nchi za Afrika wakitumia mtumbwi katika safari ya kuelekea Ulaya

Hali mbaya ya kibinadamu haiwakabili wale wakimbizi walioko safarini tu kuelekea nchi za Ulaya, lakini hata wale wanaofanikiwa kukanyaga moja ya ardhi za nchi hizo, akthari yao wanaishi katika mazingira yasiyo ya kibinadamu kwenye kambi wanazoishi. Baada ya safari yake ya siku tano ya kuzikagua kambi za wakimbizi zilizoko nchini Ugiriki, Kamishna wa Baraza la Ulaya la Haki za Binadamu ametoa indhari katika ripoti yake mpya kuhusu mazingira mabaya na ya hali ya maafa inayowakabili wakimbizi walioko kwenye kambi na vituo vya kupokea wakimbizi na wahajiri nchini humo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hali ya wahajiri zaidi ya elfu tatu wa rika la chini ya umri wa kujitegemea kisheria na wasio na jamaa zao walioandamana nao, inatia wasiwasi. Akthari ya watoto na vijana hao wadogo wanawekwa pamoja na watu wazima kwenye maskani ya maboksi au mahema, pasina na kuwekewa taratibu zozote za kuwachunga. Wengi wao wanaishia kubakwa na kutumiwa vibaya kingono.

Baadhi ya wahajiri wa Kiafrika baada ya kuokolewa

Takwimu zisizo rasmi kuhusu hali ya wakimbizi ni kubwa zaidi kuliko zinazotolewa na mashirika ya kimataifa na ya kutetea haki za binadamu. Idadi ya wahajiri wanaoghariki baharini, wanaofariki majangwani na wanaoishia kuwa mawindo ya wafanyamagendo ya binadamu inazidi kuongezeka. Wakati familia na jamaa za watu hao wanasubiri kupata habari za wapendwa wao waliohama makwao kwenda kutafuta maisha ughaibuni, maiti zisizo na majina wala utambulisho za watu hao, zimejaa kwenye maeneo ya makaburi ya jimbo la Gauteng nchini Afrika Kusini na katika miji ya pwani ya Italia, Ugiriki au Libya. Shirika la habari la Associated Press limetangaza katika ripoti yake kuwa, katika kipindi cha baada ya mwaka 2014, jumla wahajiri 56,800 wamefariki dunia au hawajulikani waliko. Idadi hiyo ni mara mbili ya ile iliyotangazwa na Shirika la Kimataifa la Uhajiri. Kwa mujibu wa shirika hilo, hadi tarehe Mosi Oktoba idadi ya wahajiri waliofariki ilipindukia watu 28,500.

Kwa masikitiko ni kuwa, tunayoshuhudia leo hii katika nchi za Magharibi kuhusiana na namna ya kukabiliana na kadhia ya uhajiri na ukimbizi ni kupuuzwa utu na ubindamu katika kadhia hiyo. Wahajiri na wakimbizi hao ni watu wanaotangatanga na wasio na pa kujihifadhi; kwa hivyo kuchukua hatua kali za kiusalama dhidi yao, si ufumbuzi wa tatizo lao

error: Content is protected !!