Dk. Shein: Tunaendelea kuchukua juhudi kupambana na maradhi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akiwa na wageni kutoka Mfuko wa Umoja wa Mataifa Unaoshughulikia Maendeleo ya Watoto (UNICEF). Katikati Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania Maniza Zaman na Mkuu mpya wa UNICEF Ofisi ya Zanzibar, Maha Damaj, waliofika ikulu mjini Zanzibar. (PICHA NA IKULU).

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameeleza mikakati inayochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kupambana na maradhi yakiwemo ya miripuko ambapo yanapozuka huathiri watu wa rika zote wakiwemo watoto.

Dk. Shein aliyasema hayo jana Ikulu, wakati alipokuwa na mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Maniza Zaman, aliyefuatana na Mkuu mpya wa shirika hilo Zanzibar, Maha Damaj, ambaye alifika kujitambulisha kwa Rais.

Alieleza kuwa miongoni mwa juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na serikali ni pamoja na kujenga mitaro mikubwa ambayo itaisadia kuondosha maji yanayotuama ambayo husababisha maradhi.

Aliongeza kuwa katika kipindi kifupi cha mradi huo, tayari umeanza kuleta matumaini ambapo athari mbali mbali ambazo awali zilikuwa zikitokea zimepungua ikiwemo kutuama kwa maji pamoja na kuleta mafuriko.

Aidha, alieleza kuwa mbali ya jitihada hizo suala zima la elimu pamoja na kuendeleza sera na mikakati ya serikali katika kupambana na maradhi pamoja na kuimarisha ustawi wa akina mama na watoto zinachukuliwa.

Alitumia fursa hiyo kuipongeza UNICEF kwa jitihada zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha watoto wa Zanzibar wanapata haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na elimu, afya na huduma nyengine za kijamii.

Alieleza kuwa kuwepo kwa Programu ya Pamoja ya Zanzibar (ZIP), inayohusisha Mashirika tisa ya Umoja wa Mataifa iliyozinduliwa hivi karibuni itasaida katika kuleta mafanikio yaliokusudiwa kwa wananchi wa Zanzibar.

Nae Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania, Maniza Zamani, alipongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwahudumia watoto pamoja na akina mama.

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepata mafanikio katika kuwahudumia watoto sambamba na kuhakikisha wanapata haki zao za msingi ikiwemo elimu na afya bora.

Alieleza kuwa shirika hilo linathamini juhudi hizo na limeshuhudia mafanikio na mabadiliko katika sekta za maendeleo hatua ambazo zimewawezesha watoto wa Zanzibar kupata haki zao za msingi pamoja na mahitaji yao muhimu ya kimaisha.

Alieleza azma ya programu ya pamoja ya UN Zanzibar kuwa mbali na mambo mengine pia itasaidia kupunguza vifo vya uzazi, ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Aliongeza kuwa UNICEF linachukua juhudi kuhakikisha wananchi wa ngazi ya chini wanashirikishwa kwa kuweka kamati ndogokatika jamii kuhakikisha inakwenda sambamba na mikakati iliyowekwa na shirika hilo.

 

 

 

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!