Dk. Shein ataka uingizaji dawa ufuate sheria

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na uongozi wa wizara ya Afya Zanzibar, wakati wa mkutano wa utekelezaji wa mpango kazi wa wizara ya Afya Zanzibar kwa kipindi cha Julai 2018 – Machi 2019. (PICHA NA IKULU).

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesisitiza kuwa chochote kinachoingia nchini kwa ajili ya matumizi ya binaadamu zikiwemo dawa na vyakula ni lazima zifuate sheria.

Hayo aliyasema jana ikulu ndogo Kibweni mjini Zanzibar, alipokutana na uongozi wa wizara ya afya wakati ilipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi wa wizara hiyo kwa kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019.

Alieleza kuwa ni kinyume na sheria na maadili ya dawa kuingiza, kuuza ama kuitangaza bila ya kufuata sheria na taratibu zilizopo na kueleza haja kwa wizara ya afya kulivalia njuga suala hilo kutokana na kujitokeza kwa wafanya biashara wa dawa zikiwemo za kiswahili wasiofuata taratibu zilizopo.

Alieleza kuwa hafurahishwi na tabia ya baadhi ya wafanyabiashara wa dawa wakiwemo waganga wa jadi wanaojitangaza na kuwafahamisha watu juu ya ubora wa dawa zao na kueleza kuwa hiyo ni kwenda kinyume na utaratibu na sheria zilizopo.

Alisema hizo ni mbinu zinazotumika kuwahadaa wagonjwa na haikubaliki si kwa Zanzibar tu hata nchi nyingi duniani kufanya biashara ya dawa namna hiyo kwani kila kitu hasa dawa hufuata taratibu na sheria zilizowekwa kulingana na maadili ya huduma hiyo.

“Haya mambo lazima Wizara ya Afya tuyajuwe, tunapaswa kuwa na utaratibu, hivyo tuziweze vizuri sheria zetu pamoja na sera ya afya kwani hali hii ikiendelea wafanyabiashara ya dawa hasa tiba asili watakuja kutuumizia watu wetu,”alisisitiza.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa wizara ya afya kwa kutekeleza vyema majukumu yao na kueleza kuwa wizara hiyo imefanya kazi nzuri.

Aliongeza kuwa ni kawaida kazi ya mwanaadamu huwa haikosi kasoro lakini hata hivyo juhudi za makusudi zimeweza kuchukuliwa na uongozi pamoja na wafanyakazi wa Wizara hiyo katika kuhakikisha mafanikio makubwa yanapatikana.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!