Dk. Magufuli atoa sababu kutowateua DPP, kamishna

RAIS John Magufuli amesema wakati wa mapendekezo ya uteuzi wa majaji jina la mkurugenzi wa mashtaka (DPP) na kamishna wa kazi yalikuwapo lakini aliamua kuachana nayo.

Magufuli alisema hayo jana ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa kuwaapisha majaji 15 wa mahakama kuu na sita wa mahakama ya rufani.

Katika hafla hiyo, walikuwapo wakurugenzi 10 wa halmashauri pamoja na wakuu wa wilaya wawili walioteuliwa Januari 27 pamoja na majaji hao.

“Sasa nikawaza DPP (Biswalo Mganga) ndiyo anayepeleka mafisadi mahakamani kwa nini nimtoe, nikaamua nimuache ili aendelee kuwapeleka”, alisema.

“Kamishna wa kazi (Gabriel Malata) naye tangu ameingia amekuwa akifanya vizuri kwa sababu kuna watu walikuwa wanapata vibali vya kazi bila kuwa na sifa lakini sasa hakuna hivyo nikaona hakuna haja ya kuwatoa”, alisema.

Alisema kazi ya kuwateua majaji hao ilikuwa ngumu hasa katika kuwahamisha watu katika vitengo vyao kuwapatia vitengo vipya kutokana na utendaji wao.

“Ndiyo maana mnaona kuna wengine wana umri mdogo hapa wengine wakubwa hadi wamebakiza mwaka mmoja kustaafu lakini mimi ndiyo mwenye jukumu la kuwaongezea miaka”, alisema Magufuli.

Amesema majaji wana nafasi kubwa ya kuwa vioo kwa jamii inayowatazama hasa wanapopewa nafasi ya kusimamia haki.

“Kazi zenu zina vishawishi vingi, lawama nyingi, inahitaji kumtanguliza Mungu ndiyo maana huwa ninasema kila mara kuwa majaji wanafanya kazi nzuri hasa wanaposimamia haki”, alisema.

Akizungumzia kitendo cha ubakaji kilichotokea wilaya ya Mufindi, Rais Magufuli alisema wakati akiangalia televisheni aliona jinsi kina mama walivyokuwa wakilalamika juu ya kuachiwa kwa mtuhumiwa aliyebaka watoto 11 bila ya kupewa hukumu yoyote.

“Kwa mujibu wa taarifa za kule, amebaka mpaka wamefikia 11 na kuachiwa na mahakama, vitu kama hivi vinawaumiza Watanzania na mimi nilitoa agizo kwa mkuu wa mkoa kuwa mtu huyo ashikwe tena waanze kusikiliza upya”, alisema.

error: Content is protected !!