China yakosoa ripoti ya Marekani kuhusu shirika la WTO

Wizara ya Biashara ya China imekosoa ripoti iliyotolewa na Marekani kuhusu Shirika la Biashara Duniani (WTO) ambayo imeituhumu Beijing kwamba inaunga mkono misimamo na hatua za upande mmoja na kuitaja ripoti hiyo kuwa isiyo na ukweli wowote.

Wizara ya Biashara ya China imetoa taarifa na kueleza kuwa ripoti hiyo ya Marekani imeandaliwa kwa mujibu wa sheria za ndani ya nchi hiyo badala ya kutayarishwa kwa mujibu wa makubaliano ya Shirika la Biashara Duniani (WTO) na sheria za pande kadhaa. Ripoti  ya Wizara ya Biashara ya China imeeleza kuwa, Beijing inaunga mkono pakubwa mfumo wa kibiashara wa pande kadhaa na mageuzi ya shirika hilo la biashara na  inapinga waziwazi hatua  na misimamo ya upande mmoja.  

Wizara ya Biashara ya China aidha imesisitiza katika taarifa hiyo kuwa, sehemu muhimu ya tuhuma za Marekani dhidi ya China  kwamba Beijing haijatimiza ahadi zake kwa WTO haina msingi wa kisheria wala hoja madhubuti. Marekani imeituhumu China kuwa inaunga mkono hatua za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja katika hali ambayo kuanzia mwezi Machi mwaka jana wa 2018 Rais Donald Trump wa Marekani yeye mwenyewe alionekana kuchukua maamuzi ya upande mmoja kwa kuanzisha vita vya kibiashara na baadhi ya nchi pale alipotangaza kuongeza  ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazongizwa nchini humo na  baadhi ya nchi ikiwemo China na nchi kadhaa za Ulaya kama chuma na alumini. Trump ambaye alikuwa akinadi nara ya “Marekani Kwanza” katika kampeni zake za uchaguzi wa rais mwaka 2016 katika kutimiza ahadi alizotoa kwa wananchi lengo likiwa ni kuunga mkono uzalishaji wa ndani aliainisha viwango vya ongezeko la ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazoingizwa Marekani na kupelekea washirika wake wa biashara ndani ya White House kukosa ushindani katika masoko ya Marekani kutokana na kukosekana ushindani wa bei za bidhaa zao.

Aidha kuna mtazamo huu kuwa, Marekani imeelekeza tuhuma zake hizo kwa China ili kuzipotosha fikra za walio wengi kuhusu taathira hatari za siasa zinazotekelezwa na White House kuhusu vita vyake hivyo vya kibiashara ilivyovianzisha kati yake na China. 

Surabi Gupta mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema: Kushtadi vita vya kibiashara kati ya Beijing na Washington ambako kunaashiria makabiliano ya kiuchumi baina ya Marekani na China zikiwa nchi mbili zenye uchumi mkubwa kunaweza kuvuga mfumo wa kibiashara wa kimataifa. 

Siasa za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekanikuhusu biashara ya kimataifa zimepelekea kuasisiwa muungano miongoni mwa nchi zilizostawi kiuchumi kwa ajili ya kukabiliana na hatua hizo za ikulu ya nchi hiyo ambazo zinakiuka kanuni na misingi ya ushindani wa kibiashara. 

Nchi wanachama wa kundi la BRICS linaloundwa na China, Russia, Brazil, India na Afrika Kusini zilitoa taarifa ya mwisho mwishoni mwa kikao chao miezi miwili iliyopita ambapo zilikosoa misimamo na hatua hizo za upande mmoja za Washington; na kutaka kuanzishwa mfumo wa kibiashara wa pande kadhaa na unaofuata sheria ambao utalinda na kudhamini biashara ya kimataifa iliyo wazi, isiyo na ubaguzi, iliyo huru na ya pamoja.  

Wakuu wa nchi wanachama wa kundi la BRICS ni kati ya shakhsia wa awali waliolalamikia na kupinga rasmi hatua za upande mmoja za Marekani kuhusu biashara ya kimataifa. Bila shaka kujitoa Marekani katika mkataba wa NAFTA na TRANS-PACIFIC pia kumetathminiwa katika fremu ya hatua zake hizo ambazo hivi sasa zimedhihirisha wazi namna White House isivyoheshimu makubaliano ya kimataifa ya pande kadhaa.

Inaonekana kuwa siasa za Marekani za kuituhumu China kwamba inachukua hatua za upande mmoja katika masuala ya kibiashara haziungwi mkono kimataifa kwa sababu kupitia siasa hizo, White House ina lengo la kuficha njama zake juu ya namna inavyovuruga na kuzuia sheria za biashara ya kimataifa.      

error: Content is protected !!