CCM yapongeza huduma za usafiri wa baharini kurejea Wete

WAJUMBE wa kamati ya siasa ya CCM mkoa wa kaskazini Pemba, wamesema ujio wa meli ya Sea Star I katika bandari ya Wete, ni jambo la kupongezwa kwani itapunguza adha ya kukimbilia bandari ya Mkoani.

Wajumbe hao walisema wananchi wa mkoa huo walikuwa wakipata tabu kwani wakati wanapohitaji usafiri walilazimika kuingia katika mabasi saa 7.00 au 8.00 usiku kuelekea bandari ya Mkoani, lakini kwa sasa tatizo hilo limeondoka.

Kauli hiyo waliitoa baada ya kupokea taarifa ya bandari ya Wete, kutoka kwa Mkuu wa bandari hiyo, wakati wajumbe wa kamati hiyo walipofanya ziara ya kuangalia utekelezaji wa ilani ya CCM na ahadi za viongozi katika Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji.

Mjumbe wa kamati hiyo, Ismail Ali Juma, alisema kulikuwa na watu waliotaka kuihujumu meli hiyo, lakini walishindwa.

Nae Omar Khamis Othaman, mjumbe wa kamati hiyo, aliutaka uongozi wa shirika la bandari Wete, kuhakikisha inaweka maboya ya kuongozea meli katika bandari hiyo.

Alisema kuna baadhi ya watu hawafurahishwi na meli hiyo kwenda katika bandari hiyo jambo ambalo linaashiria kutaka kuihujumu ili wananchi wa mkoa wa kaskazini Pemba warudi tena kwenye usumbufu.

Ofisa Mdhamini Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Hamad Ahmed Baucha, alisema, alisema mikakati ya serikali ni kuhakikisha inaimarisha  bandari hiyo, ili meli zote ziweze kufunga gati wakati wote.

Mkuu wa bandari ya Wete, Hassan Hamad, alisema shirika lina mpango wakuiongezea upana na urefu bandari hiyo, ili kuvifanya vyombo kufunga gati kwa wingi.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!